http://MIAKA 63 YA UHURU WA TANGANYIKA,WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKI KILA HATUA ZA MAENDELEO.
Na. Faraja Mbise, DDODOMA
Wananchi wameshauriwa kushiriki katika kila hatua ya maendeleo ya nchi ili kuimarisha demokrasia kwasababu wanaposhiriki katika maendeleo wanapata fursa ya kuibua changamoto na fursa zilizopo sambamba na kueleza mawazo yao na kutoa mapendekezo.
Hayo, yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mdahalo wa Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Ndugu zangu, sisi kwenye serikali, kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hata kwenye hatua ya kuweka miongozo, tunawajibika sana kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika hatua zote za kujiletea maendeleo.
Viongozi mtakubaliana na mimi hata wakati wa kupigania uhuru viongozi hawa mashuhuri tunaowasema hawakuwa pekeyao.
Hata leo kuleta maendeleo ya Tanzania hatuwezi kuwa na viongozi pasipo kuwashirikisha wananchi. Wananchi wanashirikishwa sana katika maeneo yao, kwanza kwenye kuibua vipaumbele vya maendeleo” alisema Alhaj Shekimweri.
Alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo tangu Tanzania bara ilipopata uhuru wake mpaka hivi sasa. “Natoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wetu na kuendeleza mambo mengi sana ya maendeleo yenye tija kwa nchi yetu.
Pia kujenga diplomasia na mahusiano ya kimataifa na mataifa mengine katika namna ambayo pia inaendelea kunufaisha nchi yetu. Tunamtia nguvu katika kila changamoto anayopitia kama kiongozi, najua mahitaji ya watanzania ni makubwa, najua kuna vita kubwa ya kiuchumi na kimaadili.
Lakini kwa hakika watanzania tunatambua kwamba, nchi yetu miaka 63 baada ya Uhuru, imepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo na kwamba ipo katika uelekeo mkubwa zaidi wa kufanya maendeleo makubwa zaidi”
Kuhusu mila, tamaduni na jadi zetu, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliwaasa wananchi kuzienzi na kutunza mila na tamaduni zetu. “Maana ya kuwa huru, ni kuwa na taifa lenye utambulisho wake wa mila, desturi na tamaduni zake. Na tunamuenzi Mwalimu Nyerere, hapo aliwahi kusema, ‘asiyejali mila zake ni mtumwa’. Sisi watanzania tuna tamaduni nzuri sana, mila nzuri sana, jadi nzuri sana na tunazienzi, zitambua na kuzithamini” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliwataka wananchi kulinda Uhuru wa Tanzania kwa kufanya kazi ili waweze kujitegemea kiuchumi na kuwasisitiza kuwa, hiyo ndio maana halisi ya kuwa na uhuru.
“Hakuna uhuru wa taifa kama hakuna uhuru binafsi, hatuwezi kuulinda uhuru wa taifa kama hatuwezi kulinda uhuru wetu binafsi, tujikomboe kifikra, kiuchumi ndipo tunaweza kuikomboa nchi kama taifa. Kwahiyo, tujiimarishe sana kuhakikisha kwamba tunalinda uhuru wetu.
Mwalimu Nyerere wakati ule ilikuwa Uhuru na Kazi, baadae tulipogndua kuwa kazi ni muhimu tukasema uhuru ni kazi, hapa falsafa maana yake ni nini: hatuwezi kusema tumejikomboa tuko huru kama hatufanyi kazi, lakini hapa inatukumbusha wazi kwamba, uhuru wetu utakuwa na maana pale tutakapokuwa na uwezo wa kujitegemea na utajitegemeaje ni kwa kufanya kazi kwa bidii” alisisitiza Prof. Mwamfupe.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alizungumzia maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) jinsi yalivyorahisisha suala la mawasiliano katika utendaji kazi ukilinganisha na kipindi cha nyuma wakati wa kupambania Uhuru wa Tanzania bara. “Miongoni mwa vitu ambavyo nchi yetu imepiga maendeleo makubwa sana ni kwenye teknolojia kwa maana ya matumizi ya TEHAMA.
Zamani ilikuwa unapotaka kusafiri lazima ufike stendi ukakate tiketi lakini sasahivi, huna haja ya kwenda stendi, unaweza ukafanya hivyo ukiwa nyumbani kwako. Zamani ilikuwa kama unataka kutoa au kuweka hela benki lazima uende kwenye benki na ukapange foleni, lakini siku hizi unaweza kufanya miamala kwenye simu na kwa mawakala.
Akizungumzia masuala ya mmomonyoko wa maadili, Mwanasheria wa Baraza la Machifu Mkoa wa Dodoma, Samwel Chimanyi aliwataka wananchi hasa vijana kuachana na makundi ambayo yanaathiri mifumo ya maadili ya kitanzania. “Hili eneo mkalitafsiri vizuri nyie mlioko shuleni, tuachane na kuiga makundi ambayo yamejielekeza kwenye tabia zinazoathiri mifumo ya maadili yetu. Kwahiyo, watemi wanaendelea kutoa rai na kulaani vikali masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na vitu vinavyoendelea ambayo sio vizuri kwa maadili ya kitanzania” alitoa rai Chimanyi.
Kuimarika kwa ushirikishwaji wa wananchi kutokana na mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi, mchangiaji wa mada kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nasma Ally alizungumzia kuhusu ushirikishwaji wa wanawake katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi. “Kupitia mfumo wa vyama vingi, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na mkusanyo wa mawazo katika taifa letu uliimarika. Sambamba na hilo Serikali ya Tanzania iliweza kuanzisha Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inasimamia uchaguzi wa huru na haki. Demokrasia ni haki na usawa, kwakuzingatia hilo pia, Serikali ya Tanzania iliweza kuongeza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi. Hii ilifanyika pale Tanzania ilipoongeza siti maalumu kwa wanawake.
Takwimu zinasema kutoka mwaka 1990 asilimia 4.6 zilikuwa ni kwa ajili ya wanawake Bungeni za viti maalum, kwa mwaka 2020 asilimia 36.6 ni siti maalum za wanawake. Tunapoona wanawake wanashiriki katika masuala ya nchi, hii inonesha kwamba jamii pamoja na serikali mwanamke ni kiongozi wa familia, jamii na ana mchango mkubwa sana katika kuilea jamii na kupelekea maendeleo ya taifa” alisema Ally.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Dodoma, Fatuma Madidi alichangia mada kwa kugusia maendeleo ya miundombinu katika sekta ya usafirishaji na elimu kwa kuipongeza serikali kwa kujikita katika maendeleo tangu ulipopatikana uhuru wa Tanzania bara.
“Ile dhana ya Baba wa Taifa ya kufuta ujinga imekamilika na kwamba sasa kila mmoja ana haki ya kwenda shule na kusoma.
Tanzania bara huadhimisha uhuru wake ifikapo Desemba 09 ya kila mwaka na kaulimbiu ya maadhimisho hayo ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni “Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu”.