Jumla ya Maafisa Probesheni Ishirini na Sita wamekabidhiwa kompyuta kila mmoja ili kuendana na kasi ya Uendeshaji wa Mashtaka kwa kutumia mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo sasa mfumo mpya wa teknolojia unaojulikana kama E-Case Management System ndio unaotumika nchini ikiwa ni lengo la kuharakisha mwenendo wa mashtaka mbalimbali.
Kompyuta hizo zimekabidhiwa mkoani Singida na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Kazi za Idara ya Huduma za Uangalizi ulioshirikisha Maafisa Probesheni wa mikoa ishirini na sita nchini huku wakisisitizwa kuhifadhi na kutunza vifaa hivyo sambamba na kulinda taarifa za siri zitakazokuwepo katika vifaa hivyo.
‘Naomba mvitunze vifaa mlivyopewa itakua si vizuri baada ya muda mfupi tusikie vifaa hivyo vimearibika au vimepotea lakini kumbukeni pia thamani ya hivyo vifaa inaenda sambamba na taarifa muhimu za serikali zitakazohifadhiwa humo kwahiyo nawaomba pia mvitunze ili kuepuka kuvuja kwa taarifa hizo ambazo ni nyeti sana.Niwakumbushe tu haya tunayotekeleza ni maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo ameagiza mifumo ya vyombo vyote vya haki jinai kusomana ili kuharakisha mienendo ya kesi mbalimbali.’ amesema Dkt. Maduhu