Home LOCAL DKT PHILIP ASHIRIKI MAZISHI YA BI MARGRET NTIBAYIZI

DKT PHILIP ASHIRIKI MAZISHI YA BI MARGRET NTIBAYIZI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango leo tarehe 24 Desemba 2024 ameshiriki Mazishi ya Bi. Margret Ntibayizi ambaye ni Mama wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba yaliyofanyika Mwandiga mkoani Kigoma.

Akitoa salamu za rambirambi katika msiba huo, Makamu wa Rais amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anawaombea faraja na kuungana na familia, ndugu , jamaa na marafiki katika kipindi kigumu kufuatia msiba huo.

Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba , Familia pamoja na wote walioguswa na msiba wa Bi. Margret Ntibayizi na kuwasihi kuendelea kumuombea apumzike kwa amani.

Amesema ni muhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Bi. Ntibayizi aliyoishi hapa duniani ikiwemo kwa malezi aliyotoa kwa watoto wake na mchango wake katika kusaidia ujenzi wa nyumba ya Ibada.

Makamu wa Rais amewashukuru wote waliojitokeza katika kuifariji familia wakati huu wa msiba pamoja na wale walioshiriki katika kumhudumia Bi.Margret enzi za uhai wake wakiwemo Madaktari na Viongozi wa Dini.

Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana wakati wa changamoto mbalimbali pamoja na kushiriki katika mafunzo ya kidini ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ambao umechochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, wanawake, uhalifu na mauaji.


Halikadhalika, Makamu wa Rais amewaasa Watanzania hususani vijana kuwakumbuka na kuwahudumia wazazi wao katika nyakati zote.

Previous articleHAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE TAREHE 24,DISEMBA 2024.
Next articleMALIPO YANAYOFANYWA KWA KUTUMIA MASHINE ZA POS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here