Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kupokea meli kubwa za mizigo katika bandari yake ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mafanikio baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika katika bandari hiyo uliopeleka maboresho mbalimbali ya utendaji na utoaji huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenye hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo inayoitwa EverGreen Line Group ikitokea nchini China yenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya makontena elfu nne, Meneja wa Zimamoto na Usalama wa mamlaka hiyo TPA, Mussa Biboze alisema uwekezaji na uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo umekuwa ukiwavutia wawekezaji pamoja na mawakala mbalimbali wa makampuni za meli kuleta meli zao kupitia Bandari hiyo.
“Uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Bandari ya Dar es Salaam umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji na hivyo kuvutia kampuni kama EverGreen Line Group kuleta meli yake kwenye bandari yetu,” alisema Biboze.
Alisema miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja uwepo wa kamera za ulinzi na usalama za kutosha katika eneo lote la bandari pamoja na kuongezeka kwa krane ambazo zinasaidia kushusha na kupakia makontena ndani ya muda mfupi sana, hivyo kufanya meli isitumie muda mrefu kukaa hapo bandarini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Alisema mara ya mwisho kampuni hiyo kuitumia bandari ya Dar es Salaam ilikuwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini wamerudi tena baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na wawekezaji wakiwemo DP World na Adan International Ports Holding .
Biboze alisema ujio wa meli kama hiyo utaongeza mapato kwa TPA na Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), huku ukitoa fursa kwa madereva wengi zaidi ambao watahitajika kwa ajili ya kusafirisha mizigo iliyopo ndani ya makontena hayo.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania, Mohamed Lotfy alisema hapo awali walikuwa wanaleta mizigo kupitia meli ndogo, lakini hivi sasa wameamua kuja na meli kubwa na hiyo yote ni kutokana na maboresho makubwa katika utoaji huduma yaliyofanyika katika bandari hiyo.
‘’Utafiti tulioufanya umetupa nguvu ya kuleta meli yetu kubwa ambayo ina uwezo wa kubeba makontena elfu nne.
Hivyo, tutakuwa na safari moja kila mwezi na baadae tutakuwa na safari mbili kwa mwezi ili tuweze kuleta mizigo zaidi, alisema Lotfy.
Naye Meneja Kitengo cha Biashara na Mahusiano wa Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd Donald Talawa alisema ni mafanikio makubwa kupata meli kama hiyo yenye uwezo wa kuchukua makontena mengi zaidi kwa wakati mmoja.
‘’Sisi tuko tayari kuipokea na kuihudumia meli hii ambayo ni mpya na ya kisasa ambayo imekuja moja kwa moja kutoka nchini China,”
“Napenda nikiri kwamba maboresho yaliyofanywa hapa Bandarini yanaruhusu aina ya meli kama hizi kufika kwa sababu ya kuongezwa kwa kina cha bandari’’ alieleza Talawa.
Hafla hiyo ya upokeaji wa meli hiyo pia ilihudhuriwa na Meneja Udhibiti wa Huduma za Meli kutoka katika Shirika la uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)
Fatma Masenene .
Fatma alisema ujio wa meli hiyo ni neema kwa Serikali kwa sababu inapata mapato, wamiliki wa bandari kavu, na wafanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo kama vile wa vyakula na maji na hata watu wa usafi watafaidika pia.
Meneja wa Zimamoto na Usalama kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Mussa Biboze (katikati) aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo ya ‘EverGreen Line group’ kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana, yenye uwezo wa kubeba makontena 4000. Kushoto ni Meneja kitengo cha Biashara na Mahusiano kutoka kampuni ya TEAGTL, Bw. Donald Talawa, wapili kushoto ni Bi. Fatma Masenene Meneja Udhibiti Huduma za Meli kutoka TASAC, wapili kulia ni Bw. Mohamed Lotfy Meneja kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania.
Meneja wa Zimamoto na Usalama kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Mussa Biboze (katikati) aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa akiteta jambo na Meneja wa kampuni ya usafirishaji wa makontena ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania, Bw. Mohamed Lotfy (kulia) wakati wa hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo ya kampuni hiyo kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana, kushoto ni Bi. Fatma Masenene Meneja Udhibiti Huduma za Meli kutoka TASAC.
Meneja wa Zimamoto na Usalama kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Mussa Biboze (katikati) aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa akiongoza kukata keki wakati wa hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo ya ‘EverGreen Line group’ kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana,