Home LOCAL WEKENI UTARATIBU WA KUSAJILI BIMA MASHAMBA YA MITI- WAZIRI CHANA

WEKENI UTARATIBU WA KUSAJILI BIMA MASHAMBA YA MITI- WAZIRI CHANA

Na Happiness Shayo -Mufindi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameielekeza Menejimenti ya Shamba la Miti Sao Hill kuweka utaratibu wa kujisajili katika bima kwa lengo la kukabiliana na hasara zinazotokana na miti kuungua kwa moto.

Waziri Dkt.Chana ameyasema hayo leo Novemba 25,2024 alipofanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Sao Hill lililopo Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

“Umefika wakati mkae na Taasisi zinazohusika na Bima za moto ili mjiunge kwa ajili ya kukabiliana na hasara zinazotokana na matatizo ya moto katika Shamba la Sao Hill”Mhe. Chana amesisitiza.

Aidha, Mhe. Chana ameielekeza Menejimenti hiyo kuendelea kujenga mahusiano mema na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Shamba sambamba na kufanya mikutano na wadau hasa katika Wilaya na Mikoa ili ajenda ya kudhibiti moto iwe ya kudumu.

Katika hatua nyingine Mhe. Chana ameshauri uandaaji wa maandiko ya miradi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kudhibiti na kupambana na moto.

Awali, akiwasilisha taarifa ya moto, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, Tebby Yoramu alisema kuwa moto huo ulitokea tarehe 11 Novemba 2024 na kuathiri eneo la takribani hekta 69 zenye miti katika shamba la serikali (hekta 17 miti mikubwa na hekta 52 miti midogo) na maeneo mengine yapatayo hekta takribani 430 yaliyokuwa yamevunwa kwa ajili ya maandalizi ya upandaji kwa msimu wa mwezi Januari 2025.

“Kwa upande wa wananchi inakadiriwa eneo la kati ya ekari 150 hadi 200 limeathiriwa na moto huo)” alisema Mhifadhi Tebby.

Katika kukabiliana na changamoto ya matukio ya moto kwenye shamba hilo, Mhifadhi Tebby alisema kuwa mikakati mbalimbali inaendelea kutekelezwa ikiwemo kuimarisha mahusiano mema na wadau mbalimbali, kuimarisha vikosi vya kudhibiti majanga ya moto kwa kuviongezea ujuzi ,kufanya doria za usiku na mchana, kutumia satellite pamoja na kutenga bajeti ya kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya kutambua na kupambana na moto kama drones.

http://WEKENI UTARATIBU WA KUSAJILI BIMA MASHAMBA YA MITI- WAZIRI CHANA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here