Home LOCAL WAZIRI CHANA APONGEZA UTENDAJI KAZI TANAPA, ASISITIZA UADILIFU KUFIKIA MALENGO

WAZIRI CHANA APONGEZA UTENDAJI KAZI TANAPA, ASISITIZA UADILIFU KUFIKIA MALENGO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana(Mb) ameipongeza Menejimenti na Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),kwa kazi nzuri ya uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

Ametoa pongezi hizo alipotembelea makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), leo tarehe 14,Novemba 2024 jijini, Arusha katika ziara yake ya kikazi.

“Mkakati wa kulinda maliasili ukiwa ndani ya eneo lako ndio haswa ninaoutaka na ninyi TANAPA mnatekeleza vizuri hili unapokuwa ndani ni rahisi kuwasoma majangili natoa maelekezo kwa taasisi zote chini ya wizara kuja kujifunza TANAPA na kwenda kulitekeleza hili”. alisema Balozi Chana.

Pia, Dkt.Chana alitoa rai kwa taasisi zote za wizara kuzingatia maelekezo ya mawaziri nane kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, 4R za Rais Samia na kusisitiza uadilifu kwa askari na watendaji wote na kubainisha kuwa ni jukumu kubwa la kuhifadhi ambalo walilopewa kwa niaba ya watanzania

Awali, akimkaribisha Mhe.Waziri, Kamishna wa Uhifadhi-TANAPA, Musa Nassoro Kuji alitoa ufafanuzi wa mafanikio mbalimbali ya shirika hilo ikiwemo juhudi zinazofanywa na TANAPA katika kuimarisha ulinzi na usalama wa rasilimali pamoja na wanyamapori, uboreshaji wa huduma za utalii, utekelezaji wa mfumo wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato.

“Kwa miaka minne hadi Septemba 2024, hakukuwa na tukio lolote la kuuawa kwa faru kutokana na ujangili, pia matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 15 mwaka 2016/2017 kufikia matukio matatu (3) katika mwaka 2023/2024”.

Aidha, Kamishna Kuji aliipongeza Serikali awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kujumuisha eneo la Ghuba ya Speke na kubainisha Wananchi/kaya 3,885 sawa na asilimia 91 wameshalipwa fidia zao na tayari wameshaanza zoezi la kuhama kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here