Home LOCAL WAZIRI CHANA AIPA TANO TTB KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

WAZIRI CHANA AIPA TANO TTB KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameipongeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa jitihada za kutangaza vivutio vya utalii nchini huku akisisitiza kuwa hayo ndio maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza falsafa ya 4R inayojikita katika Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

Ameyasema hayo leo Novemba 22, 2024 wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zilizopo jijini Dar es Salaam.

“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi lakini nasisitiza lazima muwe na ushirikiano katika Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili twende kwa pamoja, muende uwandani na kuvijua vivutio vilivyoko katika taasisi zote” Mhe. Chana amesisitiza.

Aidha, ameweka bayana kuwa Serikali inaitegemea bodi hiyo kuendelea kuingiza mapato hasa fedha za kigeni na kuitaka kutengeneza programu endelevu za muda mrefu za kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi na kuhakikisha tafiti za utalii zinazotolewa zinajulikana kwa taasisi zingine za Serikali ikiwemo Bunge, vyuo vikuu na nyinginezo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema kuwa TTB imejikita katika vipaumbele kadhaa ikiwemo kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa taasisi hiyo kwa kuwekeza kwenye mali za TTB na kuzalisha mapato kupitia Kituo cha Kutangaza Utalii Kiditali (DDMCC).

Ameongeza, pia TTB itajikita katika kutengeneza mgawanyiko wa kikanda wa maeneo ya vivutio vya utalii na kubuni mazao mapya ya utalii kama “Boat Cruises” sambamba na mbinu mpya za kutangaza utalii pamoja na kushawishi Waendeshaji wa Biashara ya Utalii kuhusu namna bora ya kuandaaa vifurushi vya utalii ( tourism packages ) ili kupata wageni wengi zaidi.

“ TTB imeimarisha ushirikiano kati yake na wadau mbalimbali kama vile Idara za Wizara na Serikali, Vyombo vya Habari, TRO, Mashirika ya Ndege, Hoteli, Balozi za TZ, vyama vya Utalii, na inaendelea kushawishi uwekezaji katika maeneo ya utalii kama maeneo ya vivutio (wanyamapori, utamaduni, pwani), huduma za malazi (Hoteli, kambi, Lodge n.k) uwezeshaji wa kufika katika maeneo ya utalii (mashirika ya ndege, usafiri wa ardhini nk), utalii wa matukio kama MICE Tourism, Vituo vya Burudani, mbuga za mandhari na huduma za kifedha” amesema Bw. Mafuru.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi na menejimenti ya TTB.

Previous articleUMMY MWALIMU HAPOI, AENDELEA KUWAOMBEA KURA WAGOMBEA WA CCM UCHAGUZI S/MITAA.
Next articleTIRA YATAKIWA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA SHUGHULI ZAKE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here