Home INTERNATIONAL TANZANIA,UINGEREZA WASAINI MKATABA WA HATI ,MFUKO WA AFYA WA PAMOJA.

TANZANIA,UINGEREZA WASAINI MKATABA WA HATI ,MFUKO WA AFYA WA PAMOJA.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uingereza zimesaini Mkataba wa nyongeza wa Hati ya Makubaliano ya Mfuko wa Afya wa Pamoja wenye lengo la kuimarisha huduma za afya nchini hususan Afya ya Msingi.

Mkataba huo umesainiwa Novemba 12, 2024 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba , Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (OR-TAMISEMI), Dkt. Grace Magembe na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Olukemi Williams ukishuhudiwa na Mwakilishi wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja Bi.Franziska Freiburghaus kutoka Uswisi.

Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya nchini ambapo Mwaka 1999, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo walianzisha Mfuko wa Afya wa Pamoja, ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya msingi. Fedha hizo zimekuwa zikitumika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi katika ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

“Tunawashukuru sana wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuitikia wito wa Serikali kwa kukubali kusaini mkataba wa kufadhili Mfuko wa Afya wa Pamoja. Hadi sasa wadau hao wamefikia tisa (9) ambao ni Benki ya Dunia (WB), Ireland, Uswisi, Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNPFA), Shirika la Kimataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), KOICA – Korea Kusini, Canada, Denmark na hatimaye Uingereza, baada ya kusainiwa kwa mkataba huu wa nyongeza. Siku ya leo ni sherehe kwetu baada ya kupata nyongeza ya mkataba,” amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amesema Serikali ya Uingereza itafadhili takribani Paundi za Uingereza Milioni 10 sawa na Shilingi Bilioni 31 katika kipindi cha miaka mitano ambapo kila mwaka watatoa Paundi za Uingereza Milioni 2 sawa na Shilingi Bilioni 6 za Kitanzania kwa ajili ya Mfuko huo.

“Fedha hizi zimefika wakati muafaka kwani Mfuko wa Afya wa Pamoja ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uwezo wa kutoa Huduma bora za afya nchini ambayo inakwenda sambamba na Mpango Mkakati wa Wizara ya Afya wa kuhakikisha kuwa kunakuwa na huduma bora za afya kwa wananchi wote, ikizingatiwa kuwa Serikali inaanza kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote,” Amesisitiza Dkt. Jingu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuahidi kutoa fedha hizo ambazo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kuzipeleka fedha hizo kwa watakelezaji kwa wakati hususan kwa fedha zinazokwenda katika Vituo vya kutolea huduma za afya.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Dkt. Grace Magembe amesema asilimia 90 ya fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja hutumika kuboresha huduma za afya katika ngazi ya afya ya msingi ikiwa ni pamoja na hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.

Amesema kutokana na uboreshaji wa huduma za afya kwa sasa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma katika vituo vya afya ngazi ya msingi.

Aidha, Mkurugenzi wa Maendeleo wa Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi Olukemi Williams amesema Serikali ya Uingereza ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za afya, Ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya wenye kauli mbiu ya kuhakikisha kuwa hakunab mwananchi anayeachwa nyuma bila kupata huduma bora za afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here