Home LOCAL TANZANIA KUUNGANA NA DUNIA USALAMA WA AFYA KIMATAIFA

TANZANIA KUUNGANA NA DUNIA USALAMA WA AFYA KIMATAIFA

Dkt. Biteko Ataja Jitihada za Serikali Kuboresha Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya

Dkt. Biteko Afungua Kongamano la 14 la CUHAS

Dkt. Biteko Aipongeza CUHAS kwa Tafiti na Mchango wake katika Sekta ya Afya

Wanasayansi Kuunganisha Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kwa Matokeo Bora ya Afya

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwaka 2015, Tanzania iliunga mkono Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya na kuharakisha utekelezaji wa Sheria za Afya za Kimataifa ili kuzuia magonjwa ya kuambukiza kusambaa kimataifa.

Kupitia tathimini ya pamoja ya mwaka 2023 matokeo ya maendeleo ya Tanzania katika suala hilo inaonyesha hatua kubwa ambapo mwaka 2016 imedhihirika azma imara ya Serikali katika kutekeleza Sheria za Afya za Kimataifa kwa kutumia njia moja ikikubali uunganishaji wa afya ya binadamu, wanyama, na mazingira.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 13, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la 14 la Kimataifa la Sayansi la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS) lililofanyika jijini Mwanza lenye kaulimbiu “Afya Moja na Usalama wa Afya wa Kimataifa”.

Ametaja jitihada zilizofanywa na Serikali za kuhuisha miongozo na mipango kazi ili kutekeleza Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya.
“Mwongozo wa Kitaifa wa Maabara na Usalama wa Bioteknolojia, Ajenda ya Mpango ya Kazi wa Taifa wa Usalama wa Afya, Mpango wa Mkakati wa Afya Moja (2022-2027), Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA 2023-2028). Pamoja na kuhamasisha ukuzaji na uendelezaji wa raslimali watu na kuchochea ushirikiano wa kisekta,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendea kusema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada za kuhakikisha Usalama wa Afya wa Kimataifa hasa kwa kutoa ufadhili wa masomo na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa lengo la kuongeza nguvu kazi kila mwaka.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini mchango wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya pamoja na Kituo cha Tiba cha Bugando kwa ushirikiano na washirika wa ndani na kimataifa kwa kuwa mabingwa katika nyanja mbalimbali za utafiti zinazohusiana na Usalama wa Afya wa Kimataifa,” ameeleza Dkt. Biteko.

Ameongeza “Pia Serikali inathamini mchango uliotolewa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya kuanzia mwaka 2007 hadi 2023, ambapo kimezalisha zaidi ya wataalamu wa Afya 7,000 katika fani mbalimbali za tiba, dawa, uuguzi, maabara na uchunguzi wa kiafya, na uchomaji wa mionzi ambao wamekuwa mabingwa katika Usalama wa Afya ya Kimataifa.”

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza CUHAS kwa kuandaa makongamano hayo ya kisayansi yanayojadili masuala ya kisera ili kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya na kusema kuwa afya ya binadamu inakumbwa na matishio mengi ili kukabiliana nayo ni lazima kufanya utafiti.

“Nawapongeza kwa kuleta wataalamu kwa ajili ya kujadili masuala ya tiba, niwapongeze pia kwa ugunduzi wa aina ya kirusi kinachoitwa Bugandosis ambacho kimebadilisha mfumo wa tiba na kutoa mchango katika sekta ya afya.

Fauka ya hayo amempongeza Prof. Stephen Mshana kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya kwa kuwa mwanasayansi bora kwa mwaka 2024.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya umma na binafsi hususan katika elimu na afya, akitolea mfano kupitia mradi wa Elimu ya Juu na Mabadiliko ya Uchumi (HEET).

Mradi ambao umesaidia elimu ya juu na kuwezesha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya.

Mhe. Kapanga ameongeza kuwa Afya Moja inasisitiza kutafuta suhulu ya pamoja ya changamoto ngumu za kiafya na kuwa Kongamano hilo linasaidia wataalamu, wanasayansi na watunga sera kujadiliana kwa pamoja Usalama wa Afya.

“Ni matumaini yangu tutanufaika kutokana na utaalamu na matokea ya tafiti zilizofanyika awali na mikakati itakayosaidia kupunguza matishio ya afya, nakishukuru Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya kwa kuandaa Kongamano hili,” amesema Mhe. Kipanga.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya Bugando (CUHAS), Prof. Erasmus Kamugisha amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hilo Afya Moja inalenga kuleta muunganiko wa binadamu, wanyama na afya ya mazingira ambayo inaathiri jamii, taifa na dunia katika kufikia matokeo bora ya afya.

Ameongeza kuwa Kongamano hilo linalofanyika kila mwaka limehudhuriwa na takribani washiriki 500 kutoka nchi mbalimbali duniani na litakuwa na tafiti za sayansi 150 zitakazojadiliwa kwa siku mbili.

Inaelezwa kuwa tafiti mbalimbali zinazowasilishwa kupitia makongamano hayo zimeweza kushawishi kubadilishwa kwa miongozo au sera za huduma za afya nchini ikiwemo mabadiliko ya dawa.

Aidha, kwa mwaka 2024 yamechapishwa jumla ya machapisho 271 kuhusu mada mbalimbali za tafiti.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here