Home LOCAL MAMIA WAJITOKEZA KUPIMA MACHO

MAMIA WAJITOKEZA KUPIMA MACHO

Mamia wajitokeza kupima macho Dar, waishukuru CCBRT

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ZAIDI ya wagonjwa 1,000 wa macho wengine 200 wa rufaa wamepimwa macho na kupatiwa matibabu katika zoezi linaloratibiwa na Hospital ya CCBRT katika kambi tatu tofauti Jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo ambalo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa hospitali hiyo ya CCBRT kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi.

Akizungumza na waandishi habari Jijini hapa jana wakati maandalizi ya kambi ya upimaji macho kwenye shule za msingi za Mzambarauni na Amani zilizopo Ukonga pembezoni ya mji ambako zoezi hilo litafanyika kesho baada ya lile lilofanyika kwa mafanikio makubwa kwenye Kambi ya Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa Novemba 9,2024, Dkt Sunguro Chacha amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa sana.

“Zoezi la upimaji macho kupitia kambi hiyo limekukuwa na mafanikio makubwa kwani tumeweza kubaini wagonjwa wengi wenye matatizo na kuwapa matibabu, ushauri na wengi kuwapa rufaa ya matibabu zaidi kwenye hospitali yetu iliyopo eneo la Msasani,” alisema Dkt Sunguro.

Dkt Sunguro ambaye ameambatana na Dkt Maxine Michael Harker wote kutoka Hospitali ya CCBRT amesema kambi hiyo ya siku tatu imeandaliwa kwa ushirikiano wa Hiospitali ya CCBRT na Shirika linalohusika na huduma za macho lilojulikana kama Light For The World (LFTW).

Naye Mratibu wa Kambi hizo kutoka Hospitali ya CCBRT, Bi Mariam Mchomvu amesema uhamasishaji mkubwa umefanywa na unaendelea mitaani ili wananchi zaidi wenye matatizo ya macho wajitokeze kupima afya ya macho ili kubaini tatizo mapema na waweze kupata matibabu.

“Zoezi hili la siku tatu litahitimishwa kesho kutwa(ijumaa) kwenye kambi iliyopo Shule za Msingi Mbagala Rangi Tatu na Mchikichini zote zipo Mbagala Rangi Tatu,” Bi Mariam alisema na kuongeza kuwa sambamba na zoezi hilo timu ya wataalamu kutoka CCBRT inapata fursa ya kuwabaini akina mama waliopata changamoto baadaya kujifungua (Fistula).

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Bw Deo Joseph mbali ya kuishuru Hospitali ya CCBRT, ameipongeza pia kwa kutafsiri kwa vitendo 4R za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuifanya shule yake kuwa kambi ya kudumu ya upimaji macho.

“Hii ni mara ya pili shule yangu kufanywa kambi ya upimaji macho na watoto wangu ni wanufaika wa kwanza wa huduma hii. Zoezi hili limekuwa na faida kubwa siyo kwa watoto pekee bali pia kwa jamii nzima inayotuzunguka,” alisema Mkuu wa Shule huyo Bw Joseph.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliojitokeza kupima macho, Bw Said Mwakifwamba ambaye pia ni mfanyabiashara wa matunda Kariakoo aliishukuru Hospitali ya CCBRT kwa kutoa huduma ya upimaji macho bure na matibabu yake kwa wale waliobainika kuwa na matatizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here