Home LOCAL HATUNA HURUMA TUNABEBA VYOTE – DKT. BITEKO

HATUNA HURUMA TUNABEBA VYOTE – DKT. BITEKO

*Tunataka Tuoneshe Afrika na Dunia Tanzania ni Nchi ya Demokrasia*

*Asema CCM Imejipanga Kushinda na Kuleta Maendeleo*

*Asema CCM Inataka Ushindi wa Heshima*

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa CCM chini ya uongozi wa Rais Samia imejipanga kuifanya Geita kuwa na maendeleo zaidi na katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba 27, 2024 wananchi waichague CCM na kuipa ushindi wa heshima.

Ametolea mfano wa jitihada za kuiletea maendeleo zilizofanywa na CCM kuwa ni pamoja na juhudi za Rais Samia za kuhakikisha Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) unawanufaisha zaidi wananchi kwa Geita.

Dkt. Biteko amesema hayo Novemba 24, 2024 wakati akihutubia katika Kampeni zinazoendelea za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Geita zilizofanyika katika Viwanja vya Nyankumbu mkoani Geita.

“ Sasa tunaona miradi mbalimbali ikitekelezwa, Geita maendeleo yapo kila kona tunataka mchague viongozi watakaoshirikiana na viongozi wengine ili kutuletea maendeleo, CCM tunataka ushindi wa heshima,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza “ Kwetu sisi hivi ni vyama rafiki na Mhe. Rais anaeleza kuhusu falsafa ya 4R, tunataka tuiambie Afrika na dunia kuwa Tanzania ni nchi ya demokrasia na tunafuata misingi ya waasisi wetu na sisi Geita hatuta wabagua vyama vingine lakini jambo moja hatuna huruma nalo ni kura na hatuwapi kura hata moja,”

Ameongeza “ CCM tunabeba vyote, tunabeba vijiji, vitongiji na mitaa yote hatuwaachi hata kimoja na tunafanya hivyo kwa sababu wananchi wameridhishwa na kazi kubwa ya miradi ambayo CCM imetekeleza hapa na inaendelea kutekeleza.”

Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarika kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya umeme ambayo imeongeza utoshelevu wa umeme nchini pamoja na uwepo wa treni ya umeme ambayo imeanza safari zake kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na inatarajiwa kufika Burundi hapo baadae.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu amesema kuwa Wilaya ya Geita imejipanga kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa wananchi wameona miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.

Vilevile, Kanyasu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya, elimu na barabara ambayo inaendelea vizuri.

Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mhe. Tumaini Magesa amewahimiza wananchi wa Geita kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa kuwa Serikali ya Rais Samia ina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita, Muhoja Mapande amesema kuwa wilaya yake ina vijiji 158, mitaa 65 ambapo vyama vingine vimeweka wagombea 50 na nane kati yao hawataendelea kugombea, katika vitongoji 640 vyama vingine vimeweka wagombea 115 ambapo 92 kati yao wameandika barua ya kutoaendelea na vyama hivyo.

Ameendelea kusema wagombea wa vyama hivyo wamefikia uamuzi huo baada ya kuona jitihada za CCM za kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here