Home BUSINESS TASAC YAFANYA MAZUNGUMZO NA KANALI MTAMBI KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

TASAC YAFANYA MAZUNGUMZO NA KANALI MTAMBI KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

Katika jitihada zake za kuendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kuzungumzia masuala ya usalama wa usafiri wa majini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kanali Mtambi ameipongeza TASAC kwa hatua mbalimbali wanazochukua kuimarisha masuala ya usafiri wa majini na ushirikiano wanaoutoa katika Mkoa wa Mara na hususan usalama wa wasafiri katika katika Ziwa Victoria.

Kanali Mtambi ameiomba TASAC kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni zinazohusiana na usafiri wa majini kwa wananchi na taasisi za Serikali na binafsi ili kupunguza ajali na athari za ajali za vyombo vya usafiri wa majini.

“Sisi kama Serikali tunatakiwa kuendelea kuwahakikishia usalama watumiaji wa Ziwa Victoria ikiwemo wasafiri wanaotumia vyombo vya usafiri vya majini kuhusiana na usalama wao wanapotumia usafiri wa majini,” amesema Mhe. Kanali Mtambi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira na Usafiri wa Majini, Bi. Leticia Mutaki amesema TASAC inaendelea na jukumu lake la utoaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini kwa wadau wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo taasisi na Halmashauri kuhusiana na usimamizi wa usafiri wa majini.

“Tuna mpango wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri zote zinazopakana na ziwa ili Halmashauri zisaidie kusimamia usafiri wa majini kwa niaba ya TASAC,” amesema Bi. Mutaki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Bi. Judith Kakongwe amesema Sheria na kanuni za sasa zinawabana zaidi wenye vyombo vya usafiri kuweka jaketi okozi lakini haziwabani abiria kuzivaa jambo ambalo linaleta changamoto kwa sababu wamiliki wakiweka bila kuvaliwa hazisaidii kama inatokea ajali.

“Tupo kwenye mchakato wa kubadili vipengele vya sheria na kanuni ili abiria nao wabanwe kuvaa jaketi okozi na sio tu wamiliki wa chombo kama ilivyo sasa ili kusaidia kupunguza madhara ajali zinapotokea” amesema Bi. Kakongwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here