*Masuala ya Gesi Asilia, Mafuta na Nishati Mbadala kujadiliwa*
*Kapinga aongoza ujumbe wa Tanzania*
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga ameshiriki ufunguzi wa Kongamano la Wiki ya Mafuta Afrika ( Afrika Oil Week 2024), lililofunguliwa rasmi na Waziri wa Rasilimali za Madini na Nishati wa Afrika Kusini Mhe. Gwede Mantashe.
Waziri Mantashe amesema Kongamano hilo la mwaka huu limefikisha miaka 30 tangu kuanzishwa na limekutanisha nchi zaidi ya 15 za Afrika kwa ajili ya kujadili masuala ya Mafuta, Gesi asilia na Nishati nyingine kwa ujumla.
Pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika masuala ya Nishati kongamano hilo litaangazia mikakati ya kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na uzalishaji wa kaboni na kuhamia sekta ya nishati ya kaboni kidogo.
Ufunguzi wa Kongamano hilo pia umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Kamishina wa Petroli na Gesi, Godluck Shirima na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA), Mha. Charles Sangweni.
Maudhui ya Kongamano hilo ni pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika miradi ya Mafuta, Gesi Asilia na Nishati Mbadala katika Bara la Afrika.