Home LOCAL KAMBI MAALUM YA KWANZA NCHINI YA MATIBABU KWA WAGONJWA WENYE MAUMIVU MAKALI...

KAMBI MAALUM YA KWANZA NCHINI YA MATIBABU KWA WAGONJWA WENYE MAUMIVU MAKALI KUPITIA TIBA RADIOLOJIA KUFANYIKA MUHIMBILI

Dkt. Erick Mbuguje, Bingwa Mbobezi wa Tiba Radiolojia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili akiandaa mtambo wa Angio-Suite utakaotumika katika kambi maalum kutibu wagonjwa wenye maumivu makali ya mgongo na sehemu nyingine za mwili.

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Upanga kwa kushirikiana na taasisi ya ROAD2IR ya nchini Marekani itafanya kambi maalum ya uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo na sehemu mbalimbali za mwili kwa njia ya kisasa ya tiba radiolojia itakayoongozwa na Daktari Bingwa Mbobezi wa matibabu hayo duniani Prof. David Prologo kutoka Emory Health Care ya Marekani.

Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya matibabu ambayo daktari bingwa mbobezi hutumia teknolojia ya picha za uchunguzi za (Angio-Suite, CT, Xray, Ultrasound n.k) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji.

Dkt. Erick Mbuguje, Bingwa Mbobezi wa Tiba Radiolojia MNH amesema, kambi hii itahusisha matibabu ya wagonjwa wenye maumivu makali ya aina zote yaliyogawanyika katika makundi makuu mawili; maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili.

DKt. Mbuguje amefafanua kuwa katika kundi la kwanza ni wagonjwa wenye maumivu makali ya mgongo yasiyosababishwa na saratani ni pamoja na pingili zilizosagika, kuvunjika au kupukutika ambapo matibabu ya maumivu hayo hayahusishi upasuaji, diski zinazokandamiza mishipa ya fahamu hivyo maumivu kusambaa sehemu za miguuni ambayo hayatibiki kwa upasuaji na wagonjwa wenye maumivu yatokanayo na maungio ya pingili na kuongeza kuwa kwa wagonjwa wenye maumivu ya mgongo yatokanayo na saratani iliyosababisha kuvunjika kwa pingili au kubana kwa mishipa ya fahamu nao watahudumiwa.

Dkt. Mbuguje amesema kundi la pili ni wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo vingine vya mwili ambayo hayajasababishwa na saratani kwenye magoti, mabega, nyonga ambayo matibabu ya maumivu hayo hayaondolewi kwa njia ya upasuaji na kuongeza kuwa katika kundi hili wenye maumivu mengine yatokanayo na saratani mbalimbali mfano kongosho nao pia watanufaika na huduma hiyo.

Huduma za uchunguzi na matibabu zitafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 15 Novemba, 2024, Idara ya Radiolojia iliyopo karibu na jengo la Utawala, chumba namba 24, saa 02 asubuhi hadi 11 jioni na zitatolewa kwa utaratibu wa kawaida wa hospitali. Wagonjwa wote wenye changamoto hizo wanaombwa kuwasiliana moja kwa moja na Dkt. Erick Mbuguje 0764497642, Dkt. Azza Naif 0713264350 na Dkt. Mwivano Shemwetta 0755217298 ili kupata taarifa zaidi.

Previous articleBUSHMAN SAFARI TRACKERS YATOA MSAADA WA PIKIPIKI 6 KWA ASKARI WA TAWA
Next articleMIKAKATI YA RAIS SAMIA, TANZANIA KUWA NAMBA MOJA UZALISHAJI WA CHAKULA AFRIKA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here