Home LOCAL DMDP-II KUTUMIA BIL. 290 USIMAMIZI WA TAKA NGUMU

DMDP-II KUTUMIA BIL. 290 USIMAMIZI WA TAKA NGUMU

Dar es salaam

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam Awamu ya Pili (DMDP Phase II), umepanga kutumia shilingi bilioni 290 katika uimarishaji na usimamizi wa Taka Ngumu katika Halmashauri tano za Mkoa wa Dar es salaam.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mradi wa Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyenye alipokuwa akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa DMDP awamu ya pili katika hafla ya utiaji Saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri tano za Mkoa wa Dar es salaam, katika viwanja vya Mwembeyanga, Manispaa ya Temeke.

“Gharama za utekelezaji wa mradi wa DMDP awamu ya pili ni Trilioni 1.182, asilimia 25% ya fedha za mradi sawa na shilingi bilioni 290 zitatumika katika usimamizi wa eneo la taka ngumu tofauti na awamu ya kwanza ambapo halikufanyiwa kazi katika suala la ukusanyaji, usafirishaji na kuzihifadhi taka ngumu katika madampo ya kisasa’’, alisema Mhandisi Kanyenye.

Mhandisi Kanyenye amesema mradi umewekeza nguvu katika usimamizi wa taka ngumu katika awamu ya pili ili kuboresha eneo hilo katika Mkoa wa Dar es salaam kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya ukusanyaji, usafirishaji pamoja na kuhifadhi taka ngumu katika madampo ya kisasa tofauti na awamu ya kwanza ambapo mradi ulijikita katika ununuzi wa magari na ujenzi wa vizimba.

Pia, Mhandisi Kanyenye amesema, Mradi utaboresha program mbalimbali za usimamizi wa taka ngumu ikiwemo kandarasi za ukusanyaji wa taka ngumu na kuchochea urejeshaji wa taka ngumu (Recycling), ameongeza kuwa mradi utasaidia kuanzishwa kwa taasisi ya mashirikiano ya Halmashauri zote tano za Mkoa wa Dar es salaam ambayo itasimamia taka ngumu tofauti na sasa ambapo kila Halmashauri ina utaratibu wake wa usimamizi jambo linalopelekea kukosekana kwa ufanisi wa usimamizi wa taka ngumu.

“Katika mradi huu wa Uendelezaji Jiji la Dar es salaam Awamu ya pili, madampo matatu ya kisasa yatajengwa ili kukabiliana na usimamizi wa taka ngumu katika Halmashauri zote tano katika Mkoa wa Dar es salaam na hivyo kuongeza ajira pamoja na ukuzaji wa uchumi kwa wananchi wa Mkoa Dar es salaam”, aliongeza.

Aidha, Katika awamu ya kwanza ya Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam katika eneo la usimamizi wa taka jumla ya magari 20 ya ukusanyaji taka ngumu yalinunuliwa pamoja na vizimba 65 vilijengwa, katika awamu ya pili mradi utajenga madampo matatu ya kisasa na utajikita katika ukusanyaji, usafirishaji na kuzihifadhi tofauti na hapo awali.

Mradi wa DMDP awamu ya pili unatekelezwa na TARURA kwa kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), kupitia timu ya uratibu na timu za utekelezaji zilizopo katika Halmashauri zote tano za Jiji la Dar es salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here