Home LOCAL DKT.SAMIA AMEZINDUA KITABU CHA HISTORIA MIAKA 60  YA MWENGE  WA UHURU

DKT.SAMIA AMEZINDUA KITABU CHA HISTORIA MIAKA 60  YA MWENGE  WA UHURU

Leo, Oktoba 14, 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongoza uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mwenge huo kwa historia ya Tanzania, na akabainisha kuwa historia ya Mwenge wa Uhuru haiwezi kutenganishwa na historia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kuna historia kubwa sana katika Taifa letu, na historia hiyo haiwezi kutenganishwa na historia ya Mwalimu Nyerere. Nina furaha kwamba leo tumezindua rasmi kitabu cha historia na falsafa ya Mwenge wa Uhuru, kinachoelezea misingi na historia ya mwenge huu. Tunamshukuru Hayati Balozi Job Lusinde kwa kutuachia kumbukumbu hii adhimu, Mwenyezi Mungu amrehemu mzalendo wetu huyu,” alisema Rais Samia.

Akiendelea, Rais Samia aliwapongeza wote waliofanikisha kukamilika kwa kitabu hicho, akisema kuwa kupitia kitabu hicho Watanzania watapata fursa ya kuelewa jinsi Mwenge wa Uhuru ulivyoanzishwa kabla ya Uhuru na mchango wake kwa Taifa katika vipindi mbalimbali vya kihistoria.

Nawashukuru wote waliowezesha kitabu hiki kukamilika. Kupitia kitabu hiki tunapata kufahamu namna ambavyo Mwenge wa Uhuru ulivyoasisiwa na jinsi ulivyoendelea kuangazia maisha ya Watanzania katika nyakati tofauti za mapito ya Taifa letu,” aliongeza Rais Samia.

Rais Samia pia alibainisha kuwa kitabu hicho kinatoa mwanga juu ya nafasi ya vijana katika mbio za mwenge kama tunu aliyoiacha Mwalimu Nyerere, na kwamba kitabu hicho kinaendelea kuimarisha na kulinda tunu ya Taifa.

Akizungumzia miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, Rais Samia alisema, “Mwenge wetu wa Uhuru umetimiza miaka 60. Falsafa hii imeendelea kufanya kazi na kutekeleza dhamira ya kuasisiwa kwake. Ingawa kuna mabadiliko makubwa duniani, bado Taifa letu linaendelea kushikilia falsafa hiyo kwa kutumia mbinu tofauti zinazoendana na mifumo mipya ya siasa na uchumi duniani.”

Uzinduzi wa kitabu hicho ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, ambao umekuwa na nafasi kubwa katika kuhamasisha maendeleo, umoja wa kitaifa, na mshikamano tangu kuasisiwa kwake na Mwalimu Julius Nyerere.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here