Home BUSINESS DC KINGALAME; WACHIMBAJI KUNUFAIKA KWA KUUZA DHAHABU (BoT)

DC KINGALAME; WACHIMBAJI KUNUFAIKA KWA KUUZA DHAHABU (BoT)

Na; Mwandishi wetu, GEITA

Mkuu wa Wilaya ya Nyangh’wale, Grace Kingalame ametoa wito kwa wachimbaji wa Madini kuuza dhahabu zao Benki Kuu ya Tanzania BoT,na kuacha tabia ya kuficha au kuuza kwa njia zisizo halali.

Amesema kuwa BoT imetangaza kununua dhahabu kwa masharti nafuu na kuweka vigezo vya kuwavutia wachimbaji ili kunufaika kutokana na bei nzuri iliyotangazwa na Benki hiyo.

DC Kingarame ameyasema hayo alipokuwa akitembelea Banda la Benki Kuu ya Tanzania BoT Oktoba 10, 2024, katika Maonesho ya saba ya Teknolojia katika sekta ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZ Bombambili mkoani Geita yanayowakutanisha wadau mbalimbali katika sekta hiyo ndani na nje ya nchi.

“Wito wangu ni kwa wachimbaji kuuza dhahabu zao BoT na waache kuficha au kuuza kinyemela. BoT imetangaza kununua dhahabu kwa masharti nafuu na wameweka vigezo vya kuwavutia wachimbaji. Mimi naamini ni wakati sahihi wa kuuza dhahabu sehemu salama, ambayo ni BoT,” alisema Kingalame.

Aidha, Kingalame aliipongeza BoT kwa kununua dhahabu kwa bei ya soko la dunia, na kusisitiza kuwa hakuna mchimbaji atakayeonewa kwenye mauzo hayo. Aliongeza kuwa ni fursa ya kipekee kwa wachimbaji kuuza dhahabu yao BoT, kwani kwa kufanya hivyo, wanachangia kujenga uchumi wa nchi huku wakihakikishiwa usalama wa soko.

Katika hatua nyingine, wananchi wa Geita wameipongeza BoT kwa kutoa elimu kuhusu matumizi na utunzaji wa fedha kupitia maonesho hayo ya saba ya Teknolojia ya Madini. 

Bw. Mapunda, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la BoT, alieleza kuwa ameridhishwa na elimu aliyopata kuhusu utunzaji wa fedha na mikopo.

“Baada ya kutembelea banda la BoT, nimepata elimu nzuri kuhusu utunzaji wa fedha na mikopo. Pia nimejifunza jinsi ya kutambua noti halali na bandia, na nimeshauri kuwepo kwa chenji ndogo ndogo kwenye ATM ili kusaidia mzunguko wa pesa,” alisema Mapunda.

Aidha, Mapunda alibainisha kuwa BoT imepokea wazo hilo na wameahidi kulifanyia kazi.

Kwa upande wake, mwananchi mwingine, Bw. Athanas, alisema kuwa amejifunza namna ya kuwaandaa watoto wao kuheshimu na kutunza pesa, huku akieleza kuwa alitumia muda mwingi kwenye banda hilo kupata maelezo muhimu.

Joshua Manga, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, alibainisha kuwa BoT ilianza kununua dhahabu tangu mwaka jana, na kwamba mwaka huu wameongeza motisha kwa wachimbaji na wauzaji wa dhahabu kwa kununua kwa bei ya soko la dunia.

“Benki Kuu imekuwa ikinunua dhahabu tangu mwaka jana, na mwaka huu tumeongeza motisha kwa wachimbaji. Tunanunua dhahabu kwa bei ya soko la dunia, hivyo tunawapatia nafasi ya kuuza kwetu kwa bei nzuri,” alisema Joshua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here