Home BUSINESS BoT YATANGAZA UKOMO MATUMIZI NOTI ZA ZAMANI

BoT YATANGAZA UKOMO MATUMIZI NOTI ZA ZAMANI

Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Ilulu Ilulu, akiwaonesha waandishi wa habari tofauti ya noti ya Sh.10,000 ambazo (ya upande wa kushoto) itaondolewa kwenye mzunguuko katika zoezi litakalodumu kwa miezi mitatu kuanzia Januari 6 hadi Aprili 5, 2025 katika mkutano uliofanyika leo Octaba 31, 2024 katika Ofisi za Benki hiyo Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu (BoT) Ilulu Ilulu, kizungumza na Waandishi habari kwenye mkutano uliofanyika leo Octaba 31, 2024 katika Ofisi za Benki hiyo Jijini Dar es Salaam, 

Na; Lilian Ekonga, DAR ES SALAAM.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa zoezi la kubadilisha noti za zamani  litaanza rasmi Januari 6, 2025, na litadumu  kwa kipindi cha miezi mitatu hadi tarehe 5 Aprili 2025, nakwamba  baada ya hapo noti hizo  zitafika ukomo na kutokuwa  halali kwa malipo ndani na nje ya nchi.

Aidha, (BoT) imesema  zoezi hilo  litahusisha noti za shilingi ishirini (20), mia  mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shlingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024.

Akizungumza na Waandishi habari leo Octaba 31, 2024 katika Ofisi za Benki hiyo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu (BoT) Ilulu Ilulu, amesema zoezi la ubadilishwaji litafanyika kupitia Ofisi zote za Benki na matawi yake nchini, na kupitia Benki zote za Biashara.

“Baada ya tarehe hiyo mtu yoyote au taasisi yoyote inayomiliki  fedha hizo haitaruhusiwa  kuzitumia katika  kufanya  malipo popote  Duniani, na Benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko” amesema Ilulu

Ameongeza kuwa Benki Kuu inatoa rai kwa wananchi wote wenye akiba  ya noti hizo  za zamani, kuzibadilisha  au kuziweka kwenye benki yoyote ndani ya muda uliotolewa.

“Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 sura ya 197 kifungu cha 26 kimeipa Benki Kuu mamlaka pekee ya kuchapisha  noti na kusambaza  nchini Tanzania,  huku kifungu cha 28 (2) na (3) ya sheria hiyo, Benki kuu imepewa mamlaka ya kusitisha  uhalali wa fedha itakazozianisha kadiri itakavyoona inafaa” ameongeza Ilulu.

Ilulu amewataka watanzania kuacha kuuza na kununua noti chakavu mitaani kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here