Home LOCAL WATAALAMU WA KISWAHILI WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA KISWAHILI NJE YA NCHI

WATAALAMU WA KISWAHILI WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA KISWAHILI NJE YA NCHI

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka Walimu na wadau wa lugha ya Kiswahili kuona fursa za kufundisha lugha hiyo nje ya nchi kwa kuwa tayari Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya nafasi hizo nje ya nchi.

Mhe. Ndumbaro ametoa rai hiyo Septemba 18, 2024 wakati akifungua mafunzo ya Matumizi Sanifu na Fasaha ya Kiswahili kwa Walimu na wadau wa Kiswahili wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Kiswahili ni lugha ya saba duniani na ndio utambulisho wa Taifa letu. Lugha hii ni miongoni mwa lugha rasmi katika Umoja wa Afrika, Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hivyo wataalamu wanahitajika sana katika nchi hizo, ni wakati wetu Watanzania kuona fursa hizo na kunufaika nazo”, amesema Mhe. Ndumbaro.

Hata hivyo ameeelekeza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuendelea kuhuisha Kanzi Data ya wataalamu hao mara kwa mara ili ijumuishe wataalamu hao kutoka mikoa yote nchini. Aliwataka Walimu wa Manispaa ya Songea kuwa mstari wa mbele kujisajili katika kanzi data hiyo.

Awali, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolatha Mushi amesema mafunzo hayo ni utekekezaji wa mkakati wa miaka 10 wa kubidhaisha lugha hiyo ambayo umeanza mwaka 2022 ukiwa na lengo la kuwapatia wadau hao mafunzo ili waweze kuzungumza, kufundisha na kuandika Kiswahili fasaha.

Mafunzo hayo ni kuelekea Tamasha la Tatu la Utamaduni katika Mkoa wa Ruvuma litakaloanza Septemba 20 hadi 23, 2024 katika uwanja wa Majimaji Songea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here