Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonya wananchi kuacha tabia ya kuchoma misitu bali wailinde na kuihifadhi.
Ameyasema hayo leo Septemba 26, 2024 katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
“Acheni kuchoma misitu moto, na kama ni lazima uchome moto shamba linda moto usitapakae kwenda kuharibu maeneo mengine ya misitu yaliyohifadhiwa” amesisitiza Rais Samia.
Amesema wananchi wanapochoma misitu moto inaharibu misitu pamoja na miundombinu ya barabara hivyo inarudisha nyuma maendeleo.
Kuhusu changamoto ya tembo iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa, Rais Samia amesema changamoto hiyo inaendelea kupatiwa ufumbuzi na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana.