Home LOCAL JESHI LA POLISI LINATARAJIA KUADHIMISHA MIAKA 60 YA JESHI LA POLISI TANZANIA  

JESHI LA POLISI LINATARAJIA KUADHIMISHA MIAKA 60 YA JESHI LA POLISI TANZANIA  

Jeshi la Polisi nchini linatarajia kuadhimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania inayojulikana kama ‘Siku ya Jeshi la Polisi Tanzania’ Septemba 17, 2024.

Wiki ya kilele cha maadhimisho hayo itaanza Septemba 6, 2024 katika Mikoa yote chini ya usimamizi wa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kwa askari kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutembelea na kusaidia wahitaji waliopo kwenye vituo vya msaada kama vile vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wazee.

Pia kutakuwa na upimaji wa afya na utoaji wa matibabu kwa wananchi katika mikoa yote ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa
wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Jeshi la Polisi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha na mali za watu kwa kipindi cha miaka 60.

Vilevile, kutakuwa na michezo mbalimbali itakayoshirikisha wananchi, wadau mbalimbali na Askari wa Jeshi la Polisi, pia kutafanyika matembezi (Route Match) katika mikoa mbalimbali ikiwemo Makao Makuu, Mikoa na vikosi vyake na itashirikisha wananchi na wadau wengine kwa madhumuni ya kuboresha afya na kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kubaini na kuzuia uhalifu.

Sambamba na hayo, Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi watafanya mkutano wao mkuu wa mwaka wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi kwa mwaka mmoja (1) pamoja na kupitisha maazimio na mikakati mbalimbali ya kutekeleza majukumu ya Jeshi la Polisi kwa kipindi kijacho kwa ufanisi zaidi ikiwepo Muendelezo wa Maelekezo ya Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Mkutano huo utafanyika kuanzia tarehe 12 -15 Septemba, 2024 na utafunguliwa tarehe 12 Septemba, 2024 katika Shule ya Polisi Tanzania, Mkoani Kilimanjaro, ambapo mgeni rasmi katika ufunguzi huo atakuwa Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni (Mb) Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Aidha, Mkutano huo na Maadhimisho haya yatahitimishwa rasmi Septemba 17, 2024 Mkoani Kilimanjaro, Shule ya Polisi Tanzania, na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

Jeshi la Polisi linawakaribisha wananchi wote katika maadhimisho haya kwa kushiriki michezo mbalimbali kupima afya na mikutano mbalimbali ya utoaji elimu itakayokuwa ikiendelea katika Mikoa yote hapa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here