Home LOCAL JESHI LA POLISI LATOA TAHADHARI KWA WANANCHI MAANDAMANO CHADEMA

JESHI LA POLISI LATOA TAHADHARI KWA WANANCHI MAANDAMANO CHADEMA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa tahadhari kali kwa wananchi juu ya maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) siku ya Jumatatu, Septemba 23, 2024. Kamanda wa Polisi, SACP Jumanne Muliro, amesema kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku kutokana na hofu ya kuvuruga amani jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha ITV, SACP Muliro alifafanua kuwa Jeshi la Polisi limepokea taarifa rasmi kutoka CHADEMA kuhusu dhamira ya kufanya maandamano. Hata hivyo, Jeshi hilo limejibu kwa kuwataka waandaaji kusitisha mpango huo mara moja, likionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekaidi amri hiyo.

Hatuwezi kuruhusu hali ya uvunjifu wa amani kwa namna yoyote,” alisema SACP Muliro. “Tumepokea kauli mbalimbali kutoka kwa viongozi wa CHADEMA zinazoashiria nia ya kuvuruga amani, na sisi kama Jeshi la Polisi, hatutakubali hilo litokee. Tutachukua hatua stahiki za kisheria kwa yeyote atakayeshiriki kwenye maandamano hayo.”

Kamanda huyo aliendelea kusisitiza kuwa amri ya kupiga marufuku maandamano hayo imetolewa kwa maslahi ya usalama wa raia na mali zao. Alitoa wito kwa wananchi kutohudhuria maandamano hayo na badala yake waendelee na shughuli zao za kawaida.

Sisi kama Jeshi la Polisi tumeshaeleza wazi kuwa maandamano haya yamepigwa marufuku. Wananchi wanapaswa kuelewa

kuwa usalama wao unalindwa na hivyo ni muhimu kuzingatia amri hii na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuleta madhara,” aliongeza SACP Muliro.

Jeshi la Polisi limeweka wazi kwamba litachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria na kushiriki katika maandamano hayo, kwa nia ya kudumisha amani na utulivu katika jiji la Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here