Home LOCAL WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WATAKIWAKUTOA USHIRIKIANO KWA TUME NA WADAU 

WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WATAKIWAKUTOA USHIRIKIANO KWA TUME NA WADAU 

Watendaji wa uchaguzi katika mikoa ya Mara, Simiyu na Manyara wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wa uchaguzi wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa yao.

Wito huo umetolewa leo tarehe 26 Agosti, 2024 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa watendaji wa uboreshaji ngazi ya mkoa na halmashauri yaliyofanyika katika mji wa Musoma mkoani Mara.

Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanafuata maelekezo ya Tume na kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha zoezi la uboreshaji linaenda vizuri na kwa ufanisi.

Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yoyote, msisite kuwasiliana na Tume,” amesema Jaji Mwambegele.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk ambaye alifungua mafunzo kama hayo mkoani Simiyu amewataka watendaji hao kutoa ushirikiano kwa mawakala wa vyama vya siasa, asasi za kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi hilo.

Mkoani Manyara, mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa yalifunguliwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ambaye amewataka watendaji hao kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuwafundisha Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata.

Mafunzo haya yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata ili nao wakatoe mafunzo hayo kwa waendeshaji wa vifaa vya Bayometriki na Waandishi wasaidizi ambao ndiyo watakaohusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” amesisitiza Jaji Asina.

Kufanyika kwa mafunzo hayo, ni maandalizi ya kuanza kwa mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao unajumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo Agosti 26 hadi 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara. (Picha na INEC).

Washiriki wa Mafunzo yanayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mara, wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa chama cha siasa na kutunza siri wakati wa kutekeleza majukumu yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Musoma,Bi. Aristida Tarimo. Mafunzo hayo yameanza leo Agosti 26, 2024 na yamehusisha Mratibu wa Mkoa wa Uboreshaji wa Daftari, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Uchaguzi, Maafisa TEHAMA na Maafisa Ugavi wa halmashauri zote za mkoa wa Mara. (Picha na INEC).

Previous articleMSAJILI WA HAZINA AIPONGEZA TAZAMA KWA KUTOA GAWIO LA SH. BIL ION4.35 KWA SERIKALI
Next articleDCEA YATEKETEZA MASHAMBA YA BANGI ZAIDI YA EKARI 1000 MOROGORO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here