Home BUSINESS SERIKALI KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA WILLIAMSON DIAMOND KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA...

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA WILLIAMSON DIAMOND KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA BEI YA ALMASI 

Serikali kwa kushirikiana na Kampuni Williamson Diamond inaweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa bei ya madini ya almasi katika soko la Dunia kutokana na kuibuka kwa almas inayotengenezwa katika Maabara na kuongezeka kwa mahitaji ya madini mengine.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mgodi wa uchimbaji na uzalishaji wa madini ya almasi katika mgodi wa Mwadui wa Williamson Diamond Ltd (WDL) mkoani Shinyanga.

Waziri Mavunde alisema kuwa, kwasasa duniani kuna uhitajiwa madini mengine ambayo nayo yanahitajika katika sehemu mbalimbali duniani hivyo kupelekea madini kuwa katika ushindani.

Waziri Mavunde alifafanua kuwa, Tanzania ni mwanachama wa umoja wa nchi zinazozalisha almasi Afrika(ADPA), hivyo kupitia umoja huo nchi wazalishaji zimeendelea kujadili mikakati ili kurudisha thamani ya almasi katika masoko ya ununuzi na hasa katika kukabiliana na almasi ya maabara.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini Mhe.Masache Kasaka aliupongeza mgodi kwa kazi nzuri inayofanywa na Menejimenti ya Uongozi wa mgodi hususani katika jitihada walizofanya za kukabiliana na athari kwa jamii pindi bwawa la kuhifadhi maji lilipopasuka na kuitaka Menejimenti ya Mgodi kusimamia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea hapo.

Naye,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Anamringi Macha aliutaka mgodi kuendelea kujenga mahusiano mazuri na wachimbaji wadogo wanaochimba almasi pembeni ya mgodi kwa kuwashirikisha na kuwasaidia namna bora ya kufanya uchimbaji bila kuathiri maeneo yanayozunguka mgodi hii itakuwa faida kwa mgodi na mkoa kwa ujumla.

Awali , akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi,  Ndg.Ayubu Mwenda alisema mgodi unaendelea na uzalishaji changamoto kubwa ni kushuka kwa bei kutokana na kuibuka kwa almasi inayotengenezwa katika maabara ambayo inauzwa kwa bei ya chini na kuleta ushindani katika soko.

Mwenda aliongeza kuwa, mgodi unauwezo wa kuendelea kuzalisha almasi kwa kipindi cha miaka hamsini ijayo hii ni kutokana na makadirio ya mashapo yaliyopo mgodini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here