Home LOCAL AMIRI JESHI MKUU WA MAJESHI  YA ULINZI NA USALAMA AFUNGA MAZOEZI YA...

AMIRI JESHI MKUU WA MAJESHI  YA ULINZI NA USALAMA AFUNGA MAZOEZI YA MEDANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama amesema atasimamia shabaha ya kuwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)  madhubuti na lenye Maafisa na Askari wenye weledi, ari na zana bora.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati akifunga Zoezi la Medani katika kuadhimisha Miaka 60 ya JWTZ katika eneo la Pongwe Msungura, lililoko Msata. 

Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Jeshi imara zaidi litatokana na dhamira ya kweli, moyo wa kujituma na uchumi imara zaidi.  

Vile vile, Amiri Jeshi Mkuu ameitaka JWTZ kuendelea kulinda misingi ya kuanzishwa kwa Jeshi hilo na kuendelea kudumisha nidhamu, utii, uaminifu na uhodari uliopo katika Jeshi hilo.

Rais Dkt. Samia pia amesisitiza JWTZ kuendelea kuwa Jeshi la Wananchi la ukombozi la mfano kwa Afrika na Dunia kwa namna linavyoonesha uhodari, weledi na nidhamu ya kijeshi.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kushirikiana na JWTZ katika Zoezi la Medani lililojumuisha mazoezi ya baharini na nchi kavu. Aidha, amepongeza ujio wa meli kubwa ya hospitali ya kijeshi iliyotoa huduma ya vipimo na matibabu kwa wananchi takribani 8,000.

Kupitia mazoezi hayo, JWTZ imebadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za kupambana na ugaidi, uvuvi haramu, uharamia, usafirishaji haramu wa watu na madawa ya kulevya.

Sharifa B. Nyanga
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

  Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na Usalama ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt, Samia Suluhu Hassan Katika Matukio tofautitofauti Wakati wa hafla ya kufunga zoezi la medani ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Msata Mkoani Pwani leo August 23,2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Askari wa vikundi mbalimbali vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walishiriki kwenye zoezi la Medani wakati wa shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Pongwe Msungura, Msata Mkoani Pwani tarehe 23 Agosti, 2024.

      

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here