Home INTERNATIONAL AJALI YA NDEGE YAUA 18 NEPAL

AJALI YA NDEGE YAUA 18 NEPAL


Takriban watu 18 wamefariki dunia baada ya ndege kuanguka na kuwaka moto wakati ikipaa kutoka mji mkuu wa Nepal wa Kathmandu jumatano Julai 24.

Rubani wa ndege hiyo ya Saurya Airlines iliyokuwa ikifanyiwa majaribio ambaye kwa sasa anapokea matibabu hospitalini, ndiye pekee aliyenusurika katika ajali hiyo iliyohusisha watu 19 wakiwemo wafanyakazi wa kiufundi wa shirika hilo na wafanyakazi wawili.

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Nepal ina rekodi mbaya ya usalama ambayo imehusishwa na sababu nyingi kwa miaka, kuanzia hali ya hewa isiyotabirika hadi kanuni ambazo ni dhaifu.

Ndege iliyokuwa inafanyiwa majaribio ilikuwa ikielekea Pokhara, eneo maarufu la utalii.

Video zilizowekwa mtandaoni zilionyesha ndege hiyo ikiwa imefunikwa na moto na moshi. Magari ya zima moto na ya kubebea wagonjwa yalikimbizwa eneo hilo muda mfupi baadae.

Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa 11:15 saa za huko sawa na saa 05:30 dakika chache baada ya ndege kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tribhuvan, kulingana na taarifa ya kituo cha kuratibu utafutaji na uokoaji cha Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Nepal.

Taarifa iliyotolewa ilisema ndege hiyo “ilipinda kulia na kuanguka upande wa mashariki katika njia ya kurukia ndege”.

“Iliripotiwa kuwa moto huo ulidhibitiwa na kazi ya uokoaji ilianza mara moja,” iliongeza.

“Maiti za watu 18 zilichukuliwa na mtu mmoja aliyejeruhiwa aliokolewa na kupelekwa hospitali.”

Kumi na saba kati ya waliofariki ni raia wa Nepal huku mmoja akiwa ni raia wa Yemen.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here