Home BUSINESS NHC INAVYOKWENDA KUGEUZA ENEO LA URAFIKI KISASA

NHC INAVYOKWENDA KUGEUZA ENEO LA URAFIKI KISASA

 Na mwandishi wetu

UKIONA vyaelea ujue vimeundwa! Hii ndiyo methali inayoweza kuelezea hatua ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kununua eneo la Urafiki lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kwa lengo la kufanya uwekezaji mkubwa unaolenga kuboresha mandhari na maisha ya wananch.

NHC imejipatia sifa nzuri miongoni mwa Watanzania kutokana na ubunifu wake, utekelezaji, na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa nyumba bora za makazi na biashara. Katika juhudi zake za kuendeleza maeneo mbalimbali, Mei 17, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alitembelea miradi inayotekelezwa na shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ilimfikisha katika eneo la Urafiki, ambapo wakazi walionyesha furaha na matumaini baada ya kusikia habari za kukamilika kwa ununuzi wa eneo hilo.

Katika mazungumzo yake na wakazi wa Urafiki, Abdallah aliwahakikishia kuwa shirika analoliongoza limedhamiria kufanya mageuzi makubwa kwa kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa na lenye tija.

Aliweka wazi kuwa NHC ina malengo makubwa ya kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa zaidi, likiwa na miundombinu bora na fursa nyingi za kiuchumi.

Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa NHC, Muungano Saguya, alisisitiza kuwa shirika hilo limekuwa likifanya ubunifu unaoendana na mazingira pamoja na mahitaji ya wananchi,huku likizingatia sheria, miongozo, na taratibu za taasisi hiyo na nchi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa NHC ina nia ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa makazi bora na maeneo ya kufanya biashara.

“Sisi tumedhamiria kuwa njia kwa kuwapa watu makazi bora na maeneo ya kufanya biashara. Hapa Urafiki, baada ya miaka michache ijayo, patakuwa na mandhari nzuri sambamba na kuwa eneo muhimu la kiuchumi kwa NHC na mtu mmoja mmoja,” amesema Saguya.

Eneo la Urafiki lina historia ndefu ya kuwa kituo muhimu cha viwanda na makazi, likitoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.

Kwa kutambua umuhimu wake, NHC imepanga kulifanya eneo hili kuwa na thamani zaidi kupitia uwekezaji wa kisasa unaolenga maendeleo endelevu.

Uwekezaji huu utalenga kuboresha miundombinu, kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara, na kuanzisha vituo vya huduma mbalimbali.
Moja ya mikakati muhimu ya NHC ni matumizi ya teknolojia

Shirika hilo limeamua kuanzisha kituo cha kutoa na kupokea taarifa kwa lengo la kuboresha huduma zao.

Kituo hicho kitafanya kazi saa 24, hivyo kurahisisha mawasiliano na huduma kwa wananchi. Hatua hii inatarajiwa kuleta ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati.

Kwa uwekezaji huu, NHC inaonekana kujipanga kuleta mageuzi makubwa katika eneo la Urafiki, hivyo kuongeza thamani ya eneo hilo na kuboresha maisha ya wakazi wake kwa kiwango kikubwa.

Mageuzi haya yanatarajiwa kuleta maendeleo makubwa,siyo tu katika eneo hilo, bali pia katika uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Matarajio ya Wakazi wa Urafiki.

Wakizungumzia juu ya ufanisi wa NHC, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanaotarajia kunufaika na ujio wa shirika hilo wamesema wanaamini kilio chao cha muda mrefu cha kutaka makazi bora na maeneo ya kufanyia biashara kimepata suluhisho.

Hemed Salum alisema anaamini kuwa mbali ya kuwa na mandhari nzuri, atalipwa stahiki zake alizokuwa akikidai kiwanda cha Urafiki baada ya mauziano hayo ya eneo hilo.

“Nimesikia faraja sana niliposoma na kuona walionunua eneo hili ni NHC.

Hawa jamaa wana historia nzuri ya kujenga majengo na kutoza kodi inayolipika.

Tumeona nyumba walizojenga Kawe, Chang’ombe, Kigamboni na kwingineko,” anasema Hemed.

Sakina Mambo, mkazi wa Urafiki, alisema yale majengo anayoyaona kwenye maeneo mengine kupitia vyombo vya habari sasa yanaweza kuonekana katika eneo lake na ikiwezekana yeye kuishi akipewa fursa.

NHC pia wanasifika kwa kuwatua wananchi mzigo wa malipo ya kodi kwa kuwapa fursa ya kulipa kwa namna wanavyoweza kulingana na kipato chao.

Mpangaji anaweza kulipa kodi kuanzia mwezi mmoja mmoja tofauti na wenye nyumba wengi ambao wanataka mpangaji alipe miezi sita au mwaka mmoja kwa mara moja.

Halima Shekimweri, mkazi wa Ilala Boma jijini Dar es Salaam, alisema NHC imekuwa mkombozi mkubwa kwao kwa sasa wanalipa kodi nafuu na kwa muda ambao muhusika huamua kulingana na uwezo wake.

“Hizi nyumba za NHC ni kama vile zetu. Tunaweza kulipa kadri ya uwezo wako, ukiamua mwezi mmoja mmoja, miezi sita au mwaka mmoja, ni wewe tu.

Nyumba yenye vyumba viwili, choo, sehemu ya chakula na jiko unalipa 290,000.

Kule mtaani nyumba kama hii unaipata kati ya shilingi 400,000 na 500,000,” anasem Zebedayo Juma, mkazi wa Chang’ombe, alisema baada ya kupata nyumba ya NHC hana tena hofu ya kodi na muda wa kulipa.

Nyumba anayokaa ni ya kisasa na ina vyumba viwili vya kulala, choo, jiko, sehemu ya chakula na analipa shilingi 350,000 kwa mwezi.

“Ukweli, nyumba ninayoishi na kwa eneo la hapa ingekuwa mtaani ningelipa zaidi ya shilingi 500,000, tena wangenitaka nilipe kwa mwaka. Lakini NHC wananitoza kwa mwezi, jambo ambalo limenipa unafuu mkubwa wa kujiendeleza kimaisha,” alisema Joyce Shayo, mfanyabiashara katika eneo la Shekilango, alisema sehemu ya biashara ambayo angelipia zaidi ya shilingi milioni moja kwa NHC haizidi shilingi 700,000, tena anaweza kulipa kila mwezi.

Hata akikwama,anaweza kufanya nao mazungumzo na kulipa bila kudhalilishwa kwa kufukuzwa au kutolewa maneno ya maudhi.

“Ukweli, kama NHC wangekuwa na uwezo wangejenga kwenye maeneo mengi zaidi ili kuwapa unafuu wa maisha wananchi.

Tatizo bado nyumba na majengo ya biashara ni machache na hayakidhi mahitaji ya wananchi,” anasem Samuel Nyarobi anasema kwa maeneo ya mijini hivi sasa, chumba chenye choo ndani kinatozwa kati ya shilingi 100,000 hadi 150,000.

Lakini NHC gharama hiyo unapata nyumba nzuri hasa zile za zamani.
“Namuomba Rais Samia Suluhu Hassan awaongezee mtaji NHC wajenge nyumba nyingi zaidi kwa kuwa mahitaji ni makubwa hasa kutokana na gharama za nyumba na fremu za biashara kuwa kubwa na kulipa kwa mwaka au miezi sita,” anasisitiza.
________________________________________
*Ombi la Kuongezewa Mtaji kwa NHC*

Wakazi wengi wanaamini kuwa kama Serikali itaongeza nguvu kuliwezesha NHC kujenga nyumba za ghorofa nyingi kwa ajili ya kupangisha, itawasaidia wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini wasiomudu kulipa kwa miezi sita au mwaka.

Ombi la kutaka NHC iongezewe mtaji ili lipanue zaidi huduma zake liliwahi kutolewa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ziara katika miradi ya shirika hilo.

PIC ilieleza kuwa linaamini kama NHC watapatiwa fedha zaidi, wataziwekeza katika miliki zenye faida ambapo pia serikali itanufaika kwa kupata kodi.

Kaulimbiu ya “Tunalijenga Taifa” imeendelea kuongoza NHC si kwa maneno tu bali kwa vitendo, ambapo kila kukicha miji inabadilika kimwonekano kutokana na majengo mazuri yanayojengwa na shirika hili.

*Baadhi ya miradi ya NHC*

Baadhi ya miradi hiyo iliyotekelezwa kwa ajili ya makazi na biashara katika jiji la Dar es Salaam ni pamoja na Victoria Place, Eco Residence, Kigamboni Housing Estate, Mwongozo Housing Estate, Mindu plaza, Morocco Square, Kawe 711 na Mchikichini residentials Apartments.

Miradi mingine ni ya Medeli Dodoma, Levolosi na Meru Residential Apartments Arusha ambayo ilikamilika na nyumba ziliuzwa. Hali hii imeifanya manejimeti ya NHC kuwa kinara wa kuendeleza miliki ya makazi na majengo ya umma.

Miradi mingine iliyokamilika ni nyumba zaidi ya 2000 za bei nafuu katika Halmashauri za Wilaya, jengo la biashara la Rahaleo, Singida Complex, Mpanda Plaza na lile la 2D Morogoro

.Katika ziara ya hivi karibu ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) walivutiwa na uwekezaji uliofanywa na NHC eneo la Morocco, Kawe 711 na Kawe Samia Housing Scheme unaoendana na dira ya Taifa katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

Dodoma pia kuna mradi wa Iyumbu nyumba 1000 na mji wa Serikali ambapo NHC inajenga majengo nane ya Wizara mbalimbali za Serikali.

Wakazi wa Bombambili (Geita), Ilembo (Katavi), Kongwa {Mpwapwa}, Mkinga (Tanga), Mkuzo (Ruvuma), Mlole (Kigoma), Mrara (Manyara) Mtanda( Lindi) Mvomero (Morogoro) na Unyakumi (Singida} wameingia katika kaulimbiu ya NHC ya “Nyumba yangu, maisha yangu” ambapo nyumba zilizokamilika kwenye maeneo yao zinaendelea kuuzwa kwa bei nafuu.

Mwisho

Previous articleRAIS SAMIA AWAAPISHA VIONGOZI MBALIMBALI IKULU LEO
Next articleTANZANIA NA PAKISTAN KUENDELEZA USHIRIKIANO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here