MRAJIS na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, (TCDC) , Dkt. Benson Ndiege,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4,2024 jijini Dodoma kuhusu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD 2024) yanatarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 29,2024 na kufikia kilele chake Julai 6, 2024 katika viwanja vya Nanenane – Ipuli.
Na.Alex Sonna-DODOMAA
MAADHIMISHO ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD 2024) yanatarajia kufanyika kitaifa mkoani Tabora kuanzia Juni 29,2024 na kufikia kilele chake Julai 6, 2024 katika viwanja vya Nanenane – Ipuli.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2024 jijini Dodoma na Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, (TCDC) , Dkt. Benson Ndiege, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambapo amesema kuwa shughuli mbalimbali zitafanyika kwenye maonesho hayo.
Dkt.Ndiyege amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwakutanisha wadau wa ushirika wakiwemo viongozi wa ushirika, vyama vya ushirika, wadau wa ushirika na viongozi wa Serikali wanaosimamia sekta ya ushirika.
“Pia kutangaza kazi za wanaushirika, kuhabarisha umma juu ya falsafa na manufaa ya ushirika na kutoa fursa ya kujadili changamoto za kiuchumi na kijamii zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Dkt. Ndiege.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ni “Ushirika Hujenga Kesho iliyo Bora kwa Wote”.
Aidha, amesema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano, Uchangiaji Damu, Upimaji wa Afya, Kutembelea Kituo cha Watoto Yatima na kutembelea Kambi ya Wazee.
Pia kutakuwepo na burudani mbalimbali za ngoma, Mpira wa Miguu na Pete, Riadha, Mbio za Magunia na burudani nyingine.
“Maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani hutoa fursa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kutoa huduma kwa washiriki na kupelekea kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, uchumi wa Mkoa husika na Taifa kwa ujumla.
“Maadhimisho hutoa fursa kwa wadau wa Maendeleo ya Ushirika kujifunza kuhusu fursa za uwekezaji na ufanyaji biashara kupitia bidhaa na mazao yanayozalishwa kwenye Vyama vya Ushirika,” amesema Dkt. Ndiege
Amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani husaidia kuwaunganisha wanaushirika na wabia wa maendeleo toka ndani na nje ya nchi na kuviunganisha vyama vya ushirika ili kuimarisha mahusiano katika kusaidiana masuala ya kiuchumi na kijamii.
“Katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kwa mwaka huu, tunatoa wito kwa wanaushirika na wabia wa maendeleo toka ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu kuonesha bidhaa na huduma zinazotolewa katika vyama vya ushirika na wadau wake”amesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Madhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD 2024), Meja Michael Moyo, amesema kuwa ushirika umekuwa na tija kubwa nchini licha kuwepo kwa mitizamo hasi kwa baadhi ya watu.
“Maandalizi kwa ujumla yameshakamilika hivyo tunawaomba wanaushirika kujitokeza kwa wingi kuja kushirikia na kupata elimu mbalimbali katika masuala ya yanayohusu ushirika nchini, ”amesema Meja Moyo.