Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umetoa tahadhari kwa wabunifu wote nchini kutotangaza ubunifu wao kabla hawajaulinda kwa kuusajili ili wanufaike na uvumbuzi wao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka Brela, Loy Mhando kwenye mafunzo ya waandishi wa habari leo Juni, 21, 2024, mkoani Morogoro na kueleza kuwa madhara ya kutangaza bunifu kabla ya kuzisajili ni pamoja na uharamia ambapo mtu mwingine anaweza kuiba wazo na kujinufaisha huku mbunifu halisi akishindwa kupata manufaa yoyote.
Amesema kama kuna ulazima wa mbunifu kuelezea ubunifu wake, basi anapaswa kueleza kidogo tena juujuu ili kuulinda ubunifu wake na afike Brela kwa ajili ya kuwasilisha ombi la ubunifu wake kulindwa wakati anaendelea kufanyia kazi ubunifu wake ili usiibwe na mtu mwingine.
Mhando amesema wapo baadhi ya watu ambao kazi yao ni kufuatilia ubunifu wa watu wengine na kuutumia kujinufaisha kinyume cha sheria na kwamba ili kuzuia hali hiyo, ni vyema kila mbunifu akasajili ubunifu wake kwani gharama za usajili ni ndogo na kila mbunifu anaweza kumudu.
Ametaja gharama za ada za usajili wa alama ni kwamba ada ya maombi ni Sh.50,000 , ada ya kutangaza katika jarada la Hataza na alama za biashara ni Sh. 15,000, ada ya usajili ni Sh.60,000, ada ya kuhuhisha usajili ni Sh.30,000 hii hulipwa miaka Saba baada ya usajili na kila baada ya miaka kumi badae.
Aidha ametaja ada ya kuchelewa kuhuhisha usajili ambayo ni Sh. 30,000, ada ya mabadiliko ni Sh.15,000 na 20,000 ikiwa ni pamoja na ada ya kuhamisha umiliki wa alama ni Sh.50,000, ada ya Leseni ya matumizi ni Sh.50,000 na ada ya kuunganisha umiliki ambayo ni Sh 50,000.
Pia ametaja ada ya kupata Hataza ni Sh.22,000 za Kitanzania zinazolipiwa kwa awamu mbili, wakati wa kuwasilisha maombi ni Sh.12,000 baada ya kutangaza na Hataza kutopata pingamizi ni Sh. 10,000 na ada ya kila mwaka ni Sh.4,000 kwa mwaka wa kwanza na nyongeza ya Sh. 1,000 kila mwaka ma Hataza inapokwisha muda wake ada ya mabadiliko/ marekebisho ni Sh.8000 ada ya kuhuhisha Hataza baada ya miaka kumi ya mwanzo na mitano ni Sh. 12,000 amesema,” Mhando.