Home LOCAL AMEND, UBALOZI WA USWIS WAJENGA VIVUKO VYA BARABARA KUSAIDIA WANAFUNZI JIJINI TANGA

AMEND, UBALOZI WA USWIS WAJENGA VIVUKO VYA BARABARA KUSAIDIA WANAFUNZI JIJINI TANGA

Na: Mwandishi Wetu,Tanga

KATIKA jitihada za kupunguza ajali za barabarani kwa wanafunzi jijini Tanga ,Shirika la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswis wamefanikiwa kuweka miundombinu salama barabarani yenye lengo la kuhakikisha wanafunzi wanavuka salama katika safari ya kwenda na kurudi shuleni.

Miundombinu hiyo salama ya barabara imefanyika katika Shule ya Msingi Makorora pamoja na Shule ya Msingi Azimio kwa kuwekewa vivuko vya Pundamilia, njia za watembea kwa miguu pamaja na alama muhimu za usalama barabarani.

Akizungumza kuhusu mradi huo wa miundombinu salama ya barabara, Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amefafanua mradi huo umehusisha ujenzi wa njia za watembea kwa miguu, vivuko 4 vya pundamilia, matuta saba ya kupunguza mwendo kasi, alama 15 za barabarani, na michoro 16 ya usalama barabarani.

Pia wametoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi 1,694 na walimu wa shule za msingi Makorora na Azimio ndani ya mwezi tano, 2024 Tanga na Tanzania kwa ujumla.

Kalolo amesema mpango wa kuboresha miundombinu salama ya watembea kwa miguu ni sehemu ya mradi wa mwaka mmoja unaoitwa “Usalama wa Pikipiki kwa Vijana Tanzania”.

Amesisitiza mradi huo unaungwa mkono na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na una bajeti ya Sh. 424,983,396 huku akifafanua tangu Septemba 2023, shughuli nyingine za mradi zimejumuisha mafunzo ya waendesha pikipiki 300 jijini Tanga, waendesha pikipiki 253 Dodoma.

Pia kampeni a uhamasishaji kuhusu masuala ya usalama wa pikipiki, na kuanzishwa kwa ‘Kanuni za Maadili’ kwa madereva, Waendesha pikipiki 200 zaidi watapewa mafunzo jijini Tanga ifikapo Juni 2024 na tathmini ya athari za shughuli hizo zote inafanywa hivi sasa.

“Ajali za barabarani ndiyo chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 5 na 29 duniani kote nchini Tanzania na kuna zaidi ya majeruhi 330,000 wa ajali za barabarani kwa mwaka ambayo ni ya juu kuliko wastani katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara”amesema.

Amesema mradi huo wa kuokoa maisha unaonesha ajali za barabarani zinaweza kuzuilika kazi hiyo iliyoungwa mkono na Fondation Botnar na sasa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, itaendelea kupunguza ajali za barabarani na kuokoa maisha.

Ameongeza kupitia Mpango Kazi wao wa Usafiri Salama na Endelevu kwa Jiji la Tanga, wanalenga kuhakikisha kila mtoto wa Tanga anakuwa na safari salama ya kwenda na kurudi shuleni.

“Hakuna sababu ya kuchelewa kuchukua hatua hili linahitaji kuwa kipaumbele cha juu kwa watunga sera wetu na Tanga ina uwezo wa kuongoza nchi na bara letu katika kukabiliana na chanzo hiki kikibwa cha vifo kwa vijana,”alisema

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga Dalmia Mikaya aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji , amepongeza kutekelezwa kwa mradi huo wa miundombinu ya barabara katika Shule hiyo Makorora na Azimio na matamio yao ni kuona mradi wa usalama barabarani unakwenda katika shule zote za Tanga.

Pia amewaomba wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda wanafunzi dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia. Tunafahamu suala la usalama barabarani ni muhimu lakini tuweke nguvu kusimamia usalama dhidi ya ukatili wanaofanyiwa katika jamii zetu.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Ubalozi wa Uswisi Rashid Mbaramula ambaye anashughulikia Miradi amesema nchi Uswis inahistoria kubwa wa kimahusiano na Tanzania na Jiji la Tanga ni miongoni mwao huku akifafanua kuanzia mwaka 1960 Uswis imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo na imekuwa ilishiriki kikamilifu katika kufanikisha Miradi ya maendeleo.

Amesema kupitia mradi huo madereva bodaboda zaidi ya 550 wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani na kufanikiwa kwa mradi huo kunatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali huku akiwapongeza Amend kwa kazi kubwa wanayofanya ya kutoa elimu ya usalama barabarani.

Awali Inspekta wa Jeshi la Polisi Rajab Mhumbi aliyemwakilisha Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga amesema vivuko vya barabarani ambavyo vimewekwa na Amend ni vema vikalindwa na kila mmoja wetu na si jukumu la wanafunzi na walimu peke yao.

Mwisho

Previous articleSOMA MAGAZETI YA LEO JUMANNE JUNI 4 – 2024
Next articleOCEAN ROAD YAPIGA KAMBI KITUNDA UCHUNGUZI WA SARATANI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here