Home LOCAL WAFANYAKAZI KUWENI NA MATUMAINI, RAIS ATASEMA JAMBO LAKE HIVI KARIBUNI – Dkt....

WAFANYAKAZI KUWENI NA MATUMAINI, RAIS ATASEMA JAMBO LAKE HIVI KARIBUNI – Dkt. MPANGO 

Na: Georgina Misama, Maelezo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka Watanzania hususan wafanyakazi wakae kwa matumaini kuhusu suala la nyongeza ya mshahara.

Dkt. Mpango amesema hayo leo Mei 01, 2024 katika Maadhimisho ya Sherehe za Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi yaliyofanyika kitaifa mkoani Arusha ambapo alitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Hery Mkunda kwa niaba ya wafanyakazi wote Tanzania.

“Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameniagiza niwaambie wafanyakazi wa Watanzania kwamba endapo hali ya uchumi wa nchi yetu itaendelea kuwa stahimilivu kama ambavyo tathmini za Serikali na za taasisi za kimataifa zikiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimeonyesha, wafanyakazi wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni,” alisema Dkt. Mpango.

Alisema Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mishahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa na kwamba hiyo ni misingi muhimu ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine.

Akizungumzia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika kuboresha mazingira ya wafanyakazi, Mhe. Dkt. Mpango amesema serikali imeridhia mikataba ya kimataifa 8 ya kati ya 10 ya msingi kwa kuzingatia mila na desturi za watanzania na kwamba imeanza mchakato wa kuridhia mikataba mingine 6 ya Shirika la Kazi la Dunia (ILO) ambayo inajumuisha mikataba 2 ya msingi iliyobaki.

Vilevile ameongelea suala la malipo ya watumishi wa Halmashauri na kufafanua kwamba kuanzia Julai, 2024 serikali itaanza kuwalipa mshahara wafanyakazi 473 kutoka kwenye Halmashauri 101 ambazo hazina uwezo wa kuwalipa watumishi hao kwa mapata ya ndani na kwamba kiasi cha Shilingi bilioni 3.53 kimetengwa kwenye mfuko wa serikali kuu kwa ajili ya malipo hayo.

Kwa upande wa masuala ya afya, Dkt. Mpango amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kupambana na changamoto zinazomkabili mama na mtoto hivyo serikali imetoa kauli kwamba hivi sasa kina mama wanaojifungua watoto kabla ya wakati (njiti) au wanaopata changamoto za watoto na kulazimika kuwahudumia, muda huo usiwe sehemu ya likizo yao ya uzazi na badala yake watakapokamisha matibabu wapewe likizo ya uzazi kama ilivyopaswa.

Mhe. Dkt. Mpango amewapongeza wafanyakazi wote kwa juhudi kubwa wanayofanya katika maeneo yao ya kazi amesema juhudi hizo zimesaidia kusukuma mbele maendeleo ya Taifa na kutoa rai kwa wafanyakazi wachache ambao hawatimizi majukumu yao kutumia siku ya leo kujitafakari na kudhamiria kwa dhati kubadilika.

Mwisho.

Previous articleBRELA YAWASHIKA MKONO WATOTO WENYE UHITAJI – CHAKUWAMA
Next articleWAZIRI MKUU AWATAKA WAKANDARASI MIRADI YA UMWAGILIAJI KUZINGATIA UBORA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here