Na: Georgina Misama – Maelezo
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia Mhe. Dkt. Tulia Ackson amewaasa waandishi wa habari kutumia misingi ya taaluma yao katika kutumia uhuru wa vyombo vya habari.
Dkt. Tulia alisema hayo leo Mei 02, 2024 jijini Dodoma wakati akizundua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya Dunia (WPFD), ambapo wadau wa habari kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiongozwa na Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya habari wamekutana kwa siku tatu kujadili masuala ya kihabari.
Akitoa hotuba yake ya ufufunguzi Dkt. Tulia alisema wakati mijadala mbalimbali inaendelea katika maadhimisho hayo ni vizuri kutafakari ukomo wa uhuru wa vyombo vya habari hususan katika kipindi hiki ambapo vyombo vya habari vina nafasi ya kubeba ajenda mbalimbali za kitaifa likiwemo suala la mazingira na mabadiliko tabia nchi.
“Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uhuru huu uwe na mipaka, tumieni misingi ya taaluma ya habari katika uandishi mkizingatia miiko ya uandishi wa habari mnazowapelekea wananchi, msiweke mawazo yenu wenyewe katika uhabarishaji,” alisema Mhe. Dkt. Tulia.
Aliongelea pia kuhusu uandishi wa ukatili wa kijinsia ambapo aliwataka waandishi kuandika kuhusu wanaume pia badala ya kuegemea kwa wanawake na watoto peke yao bali wahamasishe na kufundisha kwamba makundi yote katika jamii yanapaswa kuwa salama aidha, waibue changamoto zilizopo kwenye jamii ili viongozi wa serikali waweze kuzishughulikia kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.
Vilevile Dkt. Tulia aliongelea changamoto ya kiuchumi inayovikabili vyombo vya habari hususan madeni kwa serikali ambapo alisema taasisi zinazodaiwa na vyombo vya habari zinapaswa kujitathmini na kuwalipa wahusika mara moja na kwamba hatua hiyo itapelekea waandishi wa habari kwenye vyombo husika kulipwa mishahara yao inayokidhi hali na kwa wakati.
Dkt. Tulia pia alizungumzia suala la waandishi wa habari za Bunge na kuwataka wahariri wa vyombo vya habari, kuchagua waandishi maalum wa kuripoti masuala ya Bunge ili mafunzo yanayotolewa na Taasisi hiyo yawe na tija kwa waandishi wanaotoa taarifa za Bunge kwa wananchi.
MWISHO