Home LOCAL JKT HAKUNA MATESO KATIKA MAFUNZO,TUNAMWANDAA KIJANA AWE MTIIFU,MWAMINIFU NA MPENDA KAZI

JKT HAKUNA MATESO KATIKA MAFUNZO,TUNAMWANDAA KIJANA AWE MTIIFU,MWAMINIFU NA MPENDA KAZI

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele,akizungumza na waandishi wa habari katika Kikosi cha Jeshi 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama Mkoani Mara.

Mkuu wa Tawi la Mafunzo na Operesheni JKT Kanali Aisha Matanza,akizungumza na waandishi wa habari katika Kikosi cha Jeshi 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama Mkoani Mara.

Kamanda wa Kikosi cha 822 KJ Rwamkoma,Luteni Kanali Gaudencia Mapunda,akiwahimiza wazazi kuwaleta watoto wao kujiunga na mafunzo ya JKT.

Na Alex Sonna-BUTIAMA
JESHI la Kujenga Taifa ( JKT) limesema hakuna mateso katika mafunzo ambayo limekuwa likiyatoa kwani kijana anaandaliwa kuwa mtiifu,mwaminifu na anaependa kazi huku likisisitiza hakuna fedha yoyote inayohitajika ili mtoto aweze kujiunga na Jeshi hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele,wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kikosi cha Jeshi 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama Mkoani Mara.
Meja Jenerali Mabele amesema vijana wanaojiunga na JKT wapo salama na wanawalea vizuri kwa mujibu wa maadili ya kitanzania.
Amesema hakuna manyanyaso yoyote kwani kila wanachofanya kipo kwa mujibu wa mafunzo na hawapo kwa ajili ya kuwatesa vijana.
Amesema kijana anayetoka JKT atakuwa na sifa tatu ambazo ni mwaminifu,mtiifu na anaependa kazi.
“Hakuna mateso ni mambo mazuri kabisa ambayo kijana akiyafuatilia tunapata kijana mzuri ambaye atalisaidia Taifa lake,”amesema Meja Jenerali Mabele
Amesema mafunzo hayo ni gharama hivyo mzazi anaweza kumchangia kijana wake lakini watakuwa wameonesha katika tovuti ya Jeshi hilo kipi anatakiwa kuchangia.
“Hakuna pesa yoyote itakayokuwa ikihitajika pesa atakayokuja nayo ni ya matumizi ya kwake yeye mwenyewe kama mzazi atampa ni ya kuja kutumia yeye akiwa ndani ya JKT kwa matumizi yake lakini akiwa ndani kuna posho kidogo huwa tunatoa kwa ajili ya sabuni na vitu vingine,”amesema Meja Jenerali Mabele
Kutokana na hali hiyo limewataka wazazi ama walezi wakiombwa fedha kutoa taarifa katika Mamlaka husika.
Pia Jeshi hilo,limesema wakati wowote kuanzia sasa litatangaza nafasi za kujiunga na Jeshi hilo kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita hivi karibuni hivyo kuwaomba waliomaliza kuchangamkia fursa hiyo hasa wanawake.
Aidha amesema kuna mafunzo ya aina mbili ya kujitolea ambayo ni miaka miwili na vijana kwa mujibu wa sheria wanaofanya kwa miezi mitatu.
Meja Jenerali Mabele amesema JKT tayari wamejitayarisha kuwahudumia wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajia kumaliza mtihani hivi karibuni na kutakiwa kujiunga kwa mujibu wa sheria.
“Kwahiyo wakati wowote kuanzia sasa tutatangaza kwamba waje kujiunga na Jeshi.Naomba niwatoe wasiwasi kumekuwepo na mambo mengi watu wakiwatisha kwenye mitandao niwahakikishie mafunzo haya ni salama kwa watoto wote wa jinsi ya kiume na kike,”amesisitiza Meja Jenerali Mabele
Amesema hivi karibuni watatangaza na wataonesha vitu ambavyo vijana wanatakiwa kwenda navyo.
Amesema pia kwenye mafunzo ya kujitolea watu wamekuwa wakidanganyika kwa kutoa fedha ili mtoto wake aweze kusaidiwa amedai hakuna fedha bali mhusika akipita katika michakato na ukakubalika hakuna pa kutoa fedha hivyo atakaombwa atoe taarifa kwa Mamlaka husika.
Kwa upande wake,Mkuu wa Tawi la Mafunzo na Operesheni JKT Kanali Aisha Matanza,amesema kuwa mafunzo yote yanayotolewa na JKT amesema kwa upande wa mafunzo ya vijana silabi na miongozo yote imetengenezwa kwa kufuata maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Mabele.
Kanali Matanza amesema jukumu lake ni kuhakikisha yale yote silabi na masomo yanatakiwa kutekelezwa kwa vijana kwa mujibu wa sheria yanatekelezwa.
Amesema ofisi yake ndio inaratibu na kusimamia kwa kufuata maelekezo kupitia mafunzo hayo wanaowafundisha huwa wanapata semina elekezi yapi wafanye na yapi hawatakiwi kufanya.
“Kwa maana hiyo hatutegemei kwamba haya mafunzo wakufunzu wataenda kinyume.Niwatoe hofu vijana hususani Wanawake JKT ni salama anachofundishwa mwanaume ndicho anachofundishwa mwanamke hakuna vitisho manyanyaso mazoezi yameratibiwa,”amesema Kanali Matanza.
Naye, Kamanda wa Kikosi cha 822 KJ Rwamkoma,Luteni Kanali Gaudencia Mapunda amewahimiza wazazi na walezi kutumia fursa ya mafunzo ya JKT kwani yana faida kubwa
Amezitaja faida hizo ni uzalendo,ujasiri na kupenda kazi kwani kila mmoja ni shuhuda kijana anaemaliza mafunzo huwa amekamilika.
“Nitumie nafasi hii kuwaasa wazazi na walezi waleteni wahudhurie mafunzo hasa wale wa kike mimi mwenyewe ni Kamanda wa kikosi na nilianza huko,”amesema Luteni Kanali Mapunda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here