Home LOCAL TANROADS RUVUMA YAANZA MATENGENEZO DARAJA LA MTO NAMIUNGO BAADA YA KUSOMBWA NA...

TANROADS RUVUMA YAANZA MATENGENEZO DARAJA LA MTO NAMIUNGO BAADA YA KUSOMBWA NA MAJI

Na Mwandishi wetu,

Tunduru

WAKALA wa barabara Tanzania(TANROADS) mkoa wa Ruvuma,imeanza kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara katika mto Namiungo  wilayani Tunduru  ambayo iliharibiwa  na mvua na kutishia kukata mawasiliano  kati ya mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine ya Lindi,Mtwara,Pwani na Dar es slaam.

Msimamizi wa matengenezo kutoka Tanroads mkoani humo Mhandisi Godfrey Robbi alisema,tarehe 29 Februari  mwaka huu mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa tatu ilisababisha maji kuvuka juu ya daraja na kupelekea  upande mmoja wa  daraja hilo kukatika na miundombinu  yake kusombwa na maji.

Alisema,kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi hasa usafirishaji wa makaa ya mawe,wamelazimika kufanya matengenezo ya haraka ili  kuruhusu shughuli za usafiri,usafirishaji  na kiuchumi ziweze kuendelea kama kawaida.

Aidha alisema,wanaendelea kufanya matengenezo    madogo kwenye maeneo mengine ya  barabara hiyo ikiwemo eneo la Matemanga-Ligunga na Majala ambayo imeharibika vibaya ili kuwezesha watumiaji wake kupita kwa urahisi.

Robbi,amewataka wananchi hasa madereva kuzingatia alama zilizowekwa  katika eneo hilo ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea na wananchi kuacha ya kufanya shughuli za kibidamu  ikiwemo kilimo ndani ya hifadhi ya barabara, kwani wanaweza kupata hasara pindi maeneo  hayo yanapohitaji kupitisha vifaa vinavyotumika kwenye matengenezo ya barabara.

Naye Mhandisi wa kampuni ya Ovans Contructions Ltd inayofanya matengenezo ya daraja hilo Azimio Mwapongo alisema, kazi inayofanyika katika eneo hilo ni kurudisha miundombinu yote iliyosombwa na maji.

Alisema,wameanza kujaza mawe kabla ya kumwaga zege ili kuunganisha  zege na lami kwa ajili ya kuzuia maji kupenya kwenye tuta la barabara na kurekebisha baadhi ya alama nyingine zilizoharibika.

Mkazi wa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru Shaibu  Kidali,ameipongeza serikali kupitia wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) kwa kuchukua hatua za haraka kurejesha miundombinu katika daraja hilo linalounganisha wilaya  ya Tunduru na mikoa jirani ya kusini.

Alisema,barabara hiyo ni muhimu  kiuchumi kwani ndiyo inategemewa kupitisha  bidhaa zinazozalishwa katika mkoa wa Ruvuma  kwenda mikoa mingine hapa nchini na wakulima wa kijiji hicho kusafirisha mazao kutoka mashambani  kwenda  sokoni kwa ajili ya kuuza.

Pia Kidali,amemuomba mkandarasi kuhakikisha anajenga daraja imara na kukamilisha kazi kwa wakati ili waweze kulitumia daraja hilo katika shughuli zao za uzalishaji mali na kuhaidi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wakati  wote wa utekelezaji wa  kazi hiyo.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Bakari Chaulani alisema,daraja hilo ni kiungo muhimu sana siyo kwa wananchi wa kata ya Namiungo tu,bali na watu wa maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru na mikoa ya kusini.

Wakati huo huo wasafiri wanaotoka mikoa ya Lindi,Mtwara,Pwani na Dar es slaam kuelekea Songea kupitia barabara  kuu ya Mangaka-Tunduru-Songea  jana walikwama njiani kwa zaidi ya masaa 9 baada ya daraja la mto Muhuwesi wilayani Tunduru kufunikwa na maji.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema,mto huo ulianza kujaa maji majira ya saa 8 mchana na  ilipofika saa 10 jioni maji yaliongezeka na kupita juu ya daraja ambapo magari na watumiaji wengine wa barabara hiyo walishindwa kuendelea na safari zao.

Juma Said mkazi wa kijiji cha Muhuwesi alisema,ilipofika saa 6.30 usiku maji yalipungua na magari yaliaanza kupita katika daraja hilo,lakini baadhi ya madereva walishindwa kuendelea na safari na kulazimika kulala kijiji hapo na wengine walilala Tunduru mjini kabla ya kuendelea na safari yao siku ya pili.

Mmoja wa abaria  aliyekuwa anasafiri na basi la kampuni ua Super Feo  kutoka Mtwara kwenda Songea ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameiomba serikali kuhakikisha inachukua hatua za haraka kumaliza changamoto hiyo.

Alisema,hiyo ni mara ya pili katika kipindi cha miezi mitatu daraja la mto Muhuwesi kuzingirwa  na maji ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwezi Februari mwaka huu.

Picha no 315 Lori la kampuni ya Ovans Contructions Ltd inayofanya  kazi ya kurejesha miundombinu ya barabara katika daraja la mto Namiungo wilayani Tunduru likimwaga mawe kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo.

Picha no 323 Msimamizi wa matengenezo ya barabara  kutoka wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Godfrey Robbi kulia,akitoa maelekezo kwa mhandisi wa kampuni ya Ovans Contructions Ltd Azimio Mwapongo  iliyopewa kazi ya kufanya matengenezo ya barabara katika mto Namiungo wilayani Tunduru ambayo miundombinu yake iliharibiwa na mvua siku ya tarehe 29 Februari mwaka huu.

Picha no 328 Msimamizi wa matengenezo ya barabara kutoka wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Godfrey Robbi na Mhandisi wa kampuni ya Ovans Contructions Ltd Azmio Mwapongo wakiangalia sehemu  zilizoharibika vibaya kutokana na mvua za masika  zinazotakiwa kufanyiwa matengenezo  katika daraja la mto Namiungo wilayani Tunduru.

Previous articleGBT YASAJILI KAMPUNI 91 ZA MICHEZO YA KUBAHATISHA
Next articleWAKURUGENZI WA HALMASHAURI KATIKA WILAYA ZA MKOA WA TABORA WAWAAGIZWA MKOA KUTENGE FEDHA KWA AJILI YA SEKTA YA ARDHI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here