Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba, (kushoto), akizungumza na Waandishi wa Habari katika hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi cha Msajili wa Hazina na Wakurugenzi wa Bodi za Taasisi ambazo serikali ina hisa chache Machi 12,2024 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchuchu, akizungumza kwenye mahojiano na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguziĀ wa Kikao Kazi cha Msajili wa Hazina na Wakurugenzi wa Bodi za Taasisi ambazo serikali ina hisa chache unafanyika kwa siku tatu katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.
Na: Hughes Dugilo, KIBAHAĀ
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba, amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho kwenye mashirika ambayo inamiliki hisa chini ya asilimia 50 ili yaweze kutoa gawio la kutosha na kuchangia kwenye mfuko mkuu wa serikali na kukuza uchumi wa Taifa.
Dkt. Mwamba ameyasema hayo Machi 12,2024 kwenye mahojiano na waandishi wa habari katika hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi cha Msajili wa Hazina na Wakurugenzi wa Bodi za Taasisi ambazo serikali ina hisa chache unafanyika kwa siku tatu katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema kuwa upo umuhimu wa kuwaweka pamoja wajumbe wa Bodi ambao wanateuliwa na serikali ili waweze kuelewa namna ambavyo mashirika ya umma yanavyotakiwa yaendeshwe pamoja na kutambua majukumu ambayo wanatakiwa kuyatekeleza.
“Ni muhimu kuwaweka pamoja wajumbe wa Bodi ili kuelewa namna Mashirika ya Umma yanavyotakiwa kuendeshwa chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina na majukumu ambayo wanatakiwa kuyaweka mbele” amesema Dkt. Mwamba.
Amesisitiza kuwa lengo ni kuwa na picha ya pamoja ili Mashirika ambayo serikali inamiliki hisa chache yaweze kuwa na tija na kuleta maslahi kwa Taifa.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Nehemiah Mchuchu, amesema kuwa Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona ongezeko kubwa la mapato yasiyo ya kikodi na kufikia asilimia 10 ndani ya miaka mitano, ambapo sasa mapato yasiyo ya kodi ni asilimia tatu.
“Tunaamini tutafika kwa sababu tumejipanga, tunaenda vizuri sana chini ya wizara zetu mbili ambazo ni Uwekezaji na Mipango, na Wizara ya Fedha, pamoja na Wizara nyingine ambazo Taasisi hizi zimekuwa zikisimamiwa kisera katika kutekeleza majukumu yao” amesema Mchechu.
Ameongeza kuwa mpaka sasa uchangiaji wa Mashirika hayo ni mzuri kwani wanachangia asilimia 50 ya makampuni yote, na kwamba kiwango wanachochangia ni kikubwa kwa wastani hata kuzidi yale mashirika yanayomilikwa na serikali kwa asilimia 100.
Mchechu ameeleza kuwa Mkutano huo ni tukio muhimu kwa wadau kwa kuweza kuelewa vipaumbele vya serikali kama mwana hisa katika kujenga uchumi wa nchi, na kwamba waweze kupata mawazo yao katika kuendesha uchumi wa nchi kwa kuchangia katika mfuko wa Serikali.