Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kuyaenzi maono ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa kusimamia ustawi wa wananchi, kutenda haki na kuwa mstahamilivu.
Rais Samia amesema hayo katika mazishi ya kitaifa ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Amani Abeid Karume.
Aidha, Rais Samia amesema kwa ustahamilivu wake wakati wa uongozi, hayati Mwinyi aliheshimu haki za binadamu na utawala bora na kuruhusu maoni tofauti yenye kuikosoa serikali.
Vile vile, Rais Samia amesema licha ya Hayati Mwinyi kuwa kiongozi katika vipindi vigumu kisiasa na kiuchumi aliweza kuhakikisha utulivu na kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Rais Samia pia amesema Hayati Mwinyi ana mchango endelevu uliozisaidia serikali za awamu zilizofuatia kwani ndiye aliyehamasisha uwekezaji kutoka sekta binafsi na soko huria zilizochangia katika ukusanyaji mapato.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Watanzania kuishi kwa kufuata misingi bora ya maisha na malezi na kuyachukulia maisha ya Hayati Mwinyi kama funzo katika kuwalea vijana kwa kuzingatia maadili ya dini na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Hayati Mwinyi ameacha alama za kudumu na za kihstoria kama Rais wa mwisho kuiongoza Tanzania katika mfumo wa chama kimoja na kuweka ukomo wa mihula ya Urais.
Zuhura Yunus,
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu