Home BUSINESS WAZIRI KAIRUKI AZINDUA VITENDEA KAZI VYA DORIA MISITUNI VYENYE THAMANI YA SHILINGI...

WAZIRI KAIRUKI AZINDUA VITENDEA KAZI VYA DORIA MISITUNI VYENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 6

• Asisitiza lengo ni kuboresha utendaji kazi

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amezindua vitendea kazi vya doria misituni vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6, huku akiwataka Maafisa na Askari Uhifadhi kutumia vifaa hivyo kwa malengo na kazi zilizokusudiwa za doria na usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki.

Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Maliasili na Utalii , jengo la Mpingo leo Februari 20,2024 jijini Dar es Salaam.

Kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha utendaji wa jeshi letu leo tunashuhudia jitihada za Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuboresha mazingira ya utendaji kwa kununua vitendea kazi hivi ambavyo ni magari maalum mawili yenye kuweza kutoa huduma hususani doria katika mazingira magumu ya msituni na pikipiki 39 zenye uwezo wa juu kiutendaji” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Waziri Kairuki ameielekeza TFS kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatunzwa ili viweze kutoa huduma bora kwa muda mrefu, TFS iweze kuonyesha mabadiliko ya usimamizi wa misitu, rasilimali nyuki na usimamizi wa mashamba ya miti nchini na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Jeshi la Uhifadhi kwa ujumla.

Aidha, Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na kutumia nishati mbadala kama vile mkaa mbadala (briquattes), gesi ili kunusuru uharibifu wa misitu na pia kujiepusha na uvamizi katika maeneo yote yaliyohifadhiwa iwe ni misitu, au maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amewataka maafisa na askari wote wa Jeshi la Uhifadhi kujiepusha na vitendo vya rushwa, uzembe na hujuma zote za mali za umma wakati Serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya utendaji, maslahi ya watumishi na kuboresha mifumo

“Mnatakiwa kufanya kazi kwa weledi na ari ya hali ya juu kwani Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kazi na dhamana kubwa mliyokabidhiwa” Mhe. Kairuki amesema.

Waziri Kairuki amewahakikishia Maafisa na Askari Uhifadhi kuwa Serikali itaendelea kuboresha utendaji kazi wao kwa kuwapatia vifaa na taaluma muhimu zinazohitajika ili kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa misitu.

Hafla hiyo pia iliambatana na kukabidhiwa na kuzinduliwa kwa magari madogo mawili (2) ambayo yamenunuliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) kwa ajili ya kusaidia jitihada za Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania katika kujenga uwezo wa kusimamia misitu yetu kwa ufanisi.

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema vifaa vilivyozinduliwa vitaimarisha jitihada za usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki nchini.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Festo Sanga, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Mkeremy, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Menejimenti ya Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here