Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Jane Kikunya akizungumza mara baada ya kupokea msaada ya kibinadamu kutoka kwa uongozi pamoja na walimu wa shule ya Msingi El-shaddai Februari 23, 2024 Jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Shule ya Msingi El-shaddai Bi. Juliana Kallinga akisoma taarifa ya msaada waliyoitoa kwa waathirika wa maporomoko ya tope, mawe na miti Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara.
Mkurugenzi Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Condrad Millinga akipokea taarifa msaada iliyosomwa na Mkurugenzi wa Shule ya Msingi El-shadai Bi. Juliana Kallinga.
Baadhi ya vitu vilivyopokelewa ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti kutoka mlima Hanang’.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
NA: MWANDISHI WETU
Uongozi wa shule ya Msingi El shaddai iliyopo Dodoma umekabidhi misaada ya kibinadamu ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti kutoka mlima Hanang’ yaliyotokea tarehe 3 Disemba 2024 mkoani Manyara.
Akipokea misaada iliyotolewa na shule hiyo tarehe 23 Februari, 2024 kwaniaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Jane Kikunya amesema Ofisi inatambua mchango mkubwa wa Taasisi zinazoendelea kushiriki katika kurejesha hali kwa waathirika wa maafa hayo kwa namna wanavyoendelea kutoa misaada mbalimbali ili kusaidia hatua ya urejeshaji hali inayoendelea.
“kipekee kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu naomba kuwashukuru kwa moyo mliouonesha na nia katika kuchangia na kutoa msaada kwaajili ya waathirika wa maafa, tunashukuru kwa Shule yenu kwa kujitokeza na kuchangia misaada muhimu kwaajili ya waathirika wa Hanang, misaada iliyotolewa itawafikia waathirika wote kwa utaratibu uliowekwa na Ofisi.”alisema Bi. Jane Kikunya.
Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kurejesha hali za waathirika wa maafa hayo yaliyosababisha vifo, uharibifu wa makazi, miundombinu ya barabara, umeme na mashamba, huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha hatua zilizopo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule hiyo Bi. Juliana Kallinga amesema uongozi wa shule na wafanyakazi wa shule hiyo wameandaa baadhi ya vitu ambavyo ni ishara ya kuwafariji waathirika hao.
“Kama familia ya El-Shaddai tunapenda kuwafariji Watanzanaia wenzetu walioathirika kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo mbalimbali kwa wakubwa na wadogo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia,lakini pia tunamuomba Mungu aendelee kuwapa mfaraja na nguvu kila aliyepotelewa na ndugu jamaa na marafiki, hakika shule yetu iliguswa na changamoto hii.”alisema Bi. Juliana.
MWISHO.