Home ENTERTAINMENTS WAZIRI KAIRUKI AHAMASISHA WADAU KUIBUA MATAMASHA KUCHAGIZA UTALII NCHINI

WAZIRI KAIRUKI AHAMASISHA WADAU KUIBUA MATAMASHA KUCHAGIZA UTALII NCHINI

Mikoa na Wilaya yatakiwa kutangaza utalii na fursa za uwekezaji.

Na: Happiness Shayo – Same

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amefungua rasmi tamasha la Utalii Same huku akihamasisha mikoa na wilaya zote nchini kuibua matamasha ya utalii na kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo yenye vivutio vya utalii lengo ikiwa ni kukuza utalii nchini.

Ameyasema hayo leo Februari 23,2024 katika ufunguzi wa tamasha hilo lenye Kaulimbiu “Alianzisha mama, Sisi tunamalizia” Wilayani Same.

“Kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Sekta ya Utalii na Ukarimu inaendelea kukua na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

“Nitumie fursa hii kuomba mikoa na halmashauri nchini kuendelea kushirikiana na wadau wa utalii katika kubuni matukio ya utangazaji utalii” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amefafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Utamaduni lililofanyika Mkoani Kilimanjaro mwaka 2022 alielekeza wadau wote wa utalii kushirikiana ili kuyaendeleza matukio ya namna hiyo katika kutangaza utalii.

Aidha, amempongeza Mheshimiwa Rais Samia kutokana na mafanikio katika Sekta ya Utalii yaliyotokana na Programu aliyoizindua ya Tanzania The Royal Tour ambapo kwa mwaka 2023 Tanzania ilitembelewa na watalii 1,808, 205 kutoka watalii 1,454,920 waliotembelea nchini mwaka huo na pia mapato yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.5 kwa mwaka 2022 hadi kufikia dola bilioni 3.34.

Ameongeza kuwa kufanyika kwa tamasha hilo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Ibara ya 67 ambayo imeelekeza kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 5 na mapato yatokanayo na utalii kufikia dola za Marekani bilioni 6.

“Ili kufikia malengo hayo ni lazima kila mmoja ahakikishe anawajibika katika nafasi yake hususani katika kutangaza utalii na fursa za uwekezaji, kutoa huduma bora kwa watalii ili waweze kurudi nchini, kuboresha miundombinu lakini pia kuendeleza uhifadhi.” Mhe. Kairuki amesema.

Aidha, Waziri Kairuki amewasihi watoa huduma walio katika mnyororo wa thamani katika Sekta ya Utalii kuhakikisha wanatoa huduma bora ili watalii watakaotembelea vivutio hivyo washawishike kurudi na kuvitangaza kwa ndugu na jamaa zao.

Waziri Kairuki ameahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kutoa ushauri wa kitaalamu kama ambavyo Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na Sheria ya Utalii Sura ya 65 inavyotaka kufanya hivyo.

Wilaya ya Same iliyopo Mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa Wilaya yenye vivutio vingi vya utalii kama Hifadhi ya Misitu ya Asilia kama Chome, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mapori ya Akiba, Mto Saseni, Maporomoko ya Mto Yongomana na Kilele cha Kwasekinga.

Previous articleSHULE YA EL-SHADDAI YAWASHIKA MKONO WATHIRIKA WA MAAFA HANANG.
Next articleWAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS SAMIA MAZISHI YA COMRED WAKASUYI TABORA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here