Home LOCAL SERIKALI KUENDELEA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MAAFA

SERIKALI KUENDELEA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MAAFA

 Na Mwandishi wetu- DODOMA

Serikali imesema imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa   ikiwemo  Kuandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino kwa kipindi cha mwezi  Septemba 2023 mpaka  mwezi Juni 2024.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 08 Februari 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mwera  Mhe. Zahor  Mohamed  Jaji aliyetaka kufahamu kuhusu  athari za mvua zilizonyesha Novemba, 2023 na mpango wa Serikali  kuzuia athari hizo kujirudia.

Mhe. Ummy ameongeza kuwa Ofsi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inaendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa katika Mikoa 18 nchini, kufuatilia mwenendo wa majanga, kutoa tahadhari kwa umma kupitia Kituo cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura.

“Ili kukabiliana na athari hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali kama vile kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia utekelezaji wa mikakati na mikataba ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo Mkakati wa Kimataifa wa Sendai wa Upunguzaji wa Athari za Maafa (2015-2030) na Mkataba wa Makubaliano wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Oparesheni za Dharura cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (2022),”Alisema Mhe. Ummy.

Akiyataja baadhi ya madhara katika yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika  kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba, 2023 hadi sasa, amebainisha kwamba ni pamoja na  mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya milipuko kwa binadamu ikiwemo kipindupindu, matukio ya radi pamoja na  upepo mkali ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.

Aidha akijibu swali kuhusu  namna Vijana wenye Ulemavu walivyonufaika na mafunzo na mikopo inayotolewa na Serikali Naibu Waziri Ummy ameeleza kwamba kwa mwaka wa fedha 2022/2023, zaidi ya vijana 2000 wamenufaika na mafunzo yanayotolewa hapa nchini kupitia  ufundi stadi na ujasiriamali katika  Vyuo vya ufundi stadi na marekebisho, vyuo vya VETA na programu ya ukuzaji ujuzi iliyopo Nchini.

“Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi cha Mwaka 2022, kiasi cha mikopo ya Shilingi bilioni 81.3 zilizotolewa kwa watu 640,723 wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu ili kuwezesha vijana wenye ulemavu kuanzisha au kuendeleza biashara zao hivyo kupunguza utegemezi,” Alifafanua Mhe. Ummy.

Previous articleKINANA ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO KUFUATIA KIFO CHA RAIS WA NAMIBIA DKT. HAGE G. GEINGOB
Next articleRAIS SAMIA ARIDHIA KUANZISHWA KWA MTAALA WA MASOMO YA UTALII
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here