Home BUSINESS PROFESA  MSAMBICHAKA  AKIPIGIA CHAPUO NEEC

PROFESA  MSAMBICHAKA  AKIPIGIA CHAPUO NEEC

Na: Mwandishi Wetu.

SERIKALI imeshauriwa kuliongezea Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) fedha ili liweze kuwahudumia Watanzania wengi.

Ushauri huo umetolewa na Mjumbe mstaafu wa Bodi ya NEEC, Profesa Lucian Msambichaka wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya saba.

Prof Msambichaka, alisema iwapo serikali itaongeza fedha NEEC itaweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kunufaisha Watanzania wengi.

“NEEC ni miongoni mwa taasisi muhimu sana katika kuhimili wa uchumi wa taifa na imefanya kazi kubwa ya kusimamia ndoto za vijana na makundi maalumu hapa nchini.

Kama serikali itawekeza nguvu kubwa na kuhakikisha baraza linakuwa na mfuko imara wa kiuchumi basi taasisi hii itasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja, makundi na taifa kwa ujumla’’alisema Prof. Msambichika.

Alisema serikali ikiliongezea uwezo baraza, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha, basi baraza litachaniga katika kutimiza ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza ushiriki wa Watanzania, hususani makundi maalum, katika shughuli za kiuchumi.

Wajumbe wapya wa bodi ni Profesa Timothy Simalenga, Theobald Sabi, Wakili Cheggy Mziray, CPA Nicodemus Mkama, Brigadia Jenerali Aloyce Mwanjile, Dk John Mduma na Dk Hamis Mwenyimvua.

Profesa Msambichaka aliwataka wajumbe kufanyakazi kwa umoja ili kufikia malengo ya baraza ya kukuza na kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa, mbali ya kuwapongeza wajumbe wapya kwa kuaminiwa ameahidi kuwa menejimenti ya NEEC itashirikiana na bodi na wadau wengine na kufanyakazi kwa bidii ili kufikia azma ya serikali ya kukuza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za kiuchumi.

Alieleza kuwa uzoefu wa baraza unaonyesha kuwa wanawake wanakimbilia mikopo wanayoichukulia kuwa ni rahisi kuipata pasipo kujua kuwa riba ni kubwa na itawarudisha nyuma kimaendeleo.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunafikisha huduma za uwezeshaji katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na kuendesha mafunzo ya elimu ya fedha, namna bora ya kutumia mifumo iliyoanzishwa na serikali sambamba na kufanya urasimishaji wa biashara za wahudumiwa,” alisema Issa na kuongeza kuwa baraza linaendelea kuratibu shughuli za wadau na kusimamia mifuko ya uwezeshaji ambayo sasa ni 72; 62 imo ndani ya serikali na 10 nje ya serikali.

Alisema NEEC imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maono na matarajio ya serikali ya awamu ya sita c yanafikiwa.
Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here