TMDA
Home BUSINESS GGML, CHEMBA YA MIGODI WAJIPANGA KUANDAA MITAALA YA WATALAAM UCHIMBAJI CHINI YA...

GGML, CHEMBA YA MIGODI WAJIPANGA KUANDAA MITAALA YA WATALAAM UCHIMBAJI CHINI YA ARIDHI

Chemba ya migodi wajipanga kuandaa mitaala ya watalaam uchimbaji chini ya ardhi

NA: MWANDISHI WETU

KATIKA kukabiliana na uhaba wa watalaam wa uchimbaji wa kina kirefu chini ya ardhi (Underground Mine), Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) kwa kushirikana na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) pamoja na wadau wengine inatarajia kutengeneza mtaala ambao utatumika kuandaa watalaam wa uchimbaji wa aina hiyo nchini.

Hatua hiyo inakuja baada ya kupita miaka 15 tangu GGML iliposhirikiana na kampuni nyingine kubwa za madini kuandaa mitaala iliyowezesha kuzalisha vijana 1,400 wa kitanzania waliobobea kwenye uchimbaji wa kina kifupi juu ya ardhi (Open Pit Mine).

Akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu wa vyuo mbalimbali 40 wanaopata mafunzo tarajali pamoja na 10 walioendelea na kupata ajira kupitia programu ya ABU katika Mgodi wa GGML mkoani Geita hivi karibuni, Katibu Mtendaji Chemba ya Migodi, Benjamini Mchwampaka alisema katika GGML na wadau hao wa madini wamejifungia jijini Mwanza kuandaa mitaala hiyo.

Amesema mitaala hiyo itatumika kuandaa vitabu ambavyo vitapelekwa katika Chuo cha ufundi stadi Veta – Moshi ili vitumike kufundishia vijana wa Kitanzania na kuzalisha watalaam wa uchimbaji wa kina kirefu chini ya ardhi (Underground Mine)

Ameongeza katika soko la madini Tanzania sasa kuna uhaba mkubwa wa watalaam hao ambao wanatakiwa kuwa na ujuzi mpana wa kuendesha mitambo ya uchimbaji wa kina kirefu chini ya ardhi.

Akizungumzia namna pengo la watalaam wa uchimbaji wa kina kifupi juu ya ardhi lililozibwa, Mchwampaka amesema shughuli za uchimbaji mkubwa zilipoanza nchini hapakuwa kabisa na taaluma ya ya kuwaandaa watalaam wa uchimbaji.

“Serikali ililazimika kuajiri watu kutoka nchi za Ghana, Mali na Afrika Kusini kuja kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na vijana wa Kitanzania.

“Kwa hiyo GGML kupitia chemba ya migodi na kampuni nyingine wakakaa chini mwaka 2009, wakachanga fedha takribani dola za marekani milioni mbili kwa ajili ya kuandaa mtaala na tukaingia makubaliano na Chuo cha VETA – Moshi kuanzisha program maalum ya miaka mitatu kuwanoa vijana kupata ujuzi uchimbaji juu ya ardhi,” amesema.

Aidha, ameipongeza GGML kwa kazi kubwa iliyoifanya kwani huo ni moja ya mradi mkubwa ambao Tanzania inajivunia kuwa na watalaam wabobevu.

Pamoja na mambo mengine amesema program iliyozinduliwa na mafunzo tarajali kwa wahitimu hao wa vyuo vikuu kwa mwaka 2024/2025 ni ushahidi tosha kwamba GGML ipo mstari wa mbele kuhakikisha vijana wa kitanzania wanaandaliwa vizuri kupata nafasi kwenye fursa za ajira.

Akizungumzia mafunzo hayo, Meneja Mwandamizi wa masuala ya rasilimali watu kutoka GGML, Charles Masubi amesema program hiyo inalenga kuwaandaa vijana kubobea katika masuala mbalimbali tofauti na waliyosomea darasani ili kukubali katika soko la ajira.

Ameongeza ili kupata wabobevu zaidi wa sekta ya madini pia GGML imeanzisha program nyingine za African Business Unit Graduate (ABU) ambayo imekwenda mbele zaidi kwa kuwapa wahitimu wa program ya mwaka mmoja kupata fursa ya kujiongezea ujuzi zaidi kutoka nchi mbalimbali ambazo kampuni mama ya AngloGold inakomiliki migodi.



LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea GGML, CHEMBA YA MIGODI WAJIPANGA KUANDAA MITAALA YA WATALAAM UCHIMBAJI CHINI YA ARIDHI