Home BUSINESS BBT YAZIDI KUKONGA MIOYO YA WATANZANIA

BBT YAZIDI KUKONGA MIOYO YA WATANZANIA

Na: Mwandishi Wetu, Njombe

WADAU mbalimbali kutoka sekta za kilimo, mifugo na uvuvi wamepongeza utekelezaji wa mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kama njia itakayosaidia kuzinua sekta hizo kupitia kundi la vijana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, mkoani Njombe, mkulima wa parachichi Fredinand Kivua amesema serikali kupitia wizara za kilimo, mifugo na uvuvi wamekuja na mpango ambao kama utasimamiwa vizuri utekelezaji wake mchango wake utaweka alama kwa uhakika wa chakula na kuinua vipato sambamba na kukuza uchumi.

“Ninaamini sisi kama wananchi tunapaswa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupititia wizara za kilimo, mifugo na uvuvi katika kuvutia vijana kujikita katika sekta hizo,”amesema Kivua.

Naye Magreth Lwangili amesema utekelezaji wa mpango wowote na hasa kipindi cha mwanzo watu huwa wanakosoa sana na kukaa pembeni kuona kama utafanikiwa lakini mafanikio yanapoonekana huanza kujisogeza na kujiweka sehemu ya mafanikio hayo.

Amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ambao umeonesha kuwavutia vijana wengi kuwekeza na kufanya shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi kwani wanategemea kutengeneza maisha yao na kupunguza umaskini katika jamii ya kitanzania.

“Sisi kama wadau wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) tunaunga mkono hatua ya serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na BBT kwani tunaamini vijana wengi wamevutiwa na mpango huo unaolemga kuleta mageuzi katika sekta husika,” amesema Lwangili.

Kwa upande wake Razack Sanga, mkulima wa mahindi Wilaya ya Makete, amesema mpango huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuwaongezea maarifa vijana juu ya kilimo biashara, na hivyo kuwaandaa kuja kushiriki kikamilifu katika kuchangia kukuza pato la taifa.

“Tunamshukuru Rais wetu kupitia wizara zake kwa kutoa fursa hii adhimu kwa vijana wetu kwani wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya kilimo biashara, ufugaji wa kisasa na bora samaki utakaochochea uzalishaji,” amesema Sanga.

Tangu mpango BBT uzinduliwe na Rais Samia mwaka jana Jijini Dodoma, mwitikio wa vijana kujiunga katika mpango huo ni mkubwa na hivyo kuongeza matumaini ya dhamira ya Tanzania kulisha Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

Mpango huo unalenga kuwezesha ushiriki wa vijana kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuhakikisha unakuwa endelevu utakao changia kuboresha na kuinua maisha ya watanzania sambamba na kutengeneza ajira milioni tatu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ifikapo mwaka 2030.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here