TMDA
Home BUSINESS ORYX YAKABIDHI MITUNGI YA GESI NA MAJIKO YAKE 700 KISARAWE,KUFUNGA MFUMO WA...

ORYX YAKABIDHI MITUNGI YA GESI NA MAJIKO YAKE 700 KISARAWE,KUFUNGA MFUMO WA GESI MINAKI SEKONDARI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo(katikati) na Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman(kushoto) wakimkabidhi mtungi wa Oryx Mwalimu wa Shule ya Msingi Kitonga Mango iliyopo wilayani Kisarawe mkoani Pwani Mkegani Mkuya ( kulia) wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko yake kwa walimu 500  wa Wilaya hiyo, lengo likiwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia .

Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Araman akifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi ya oryx 700 ambayo imekabidhiwa kwa walimu 500 pamoja na Baba na Mama Lishe 200 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani

Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (wa tatu kushoto) akimkabidhi mtungi wa gesi ya Oryx Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Seleman Jafo  ikiwa ni sehemu ya mitungi 700 iliyotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya kuigawa kwa walimu 500 pamoja na baba na mama lishe 200 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani

Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (kushoto) akifafanua jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Salemani Jafo wakati wa hafla ya kukabidhi  mitungi ya gesi ya Oryx 700 yakiwa na na majiko yake kwa walimu pamoja na baba na mama lishe katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo(kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman wakijadiliana jambo wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi ya oryx pamoja na majiko yake kwa walimu , baba lishe na mama lishe wilayani Kisarawe

Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akitoa elimu ya matumizi salama ya mtungi wa gesi kabla ya kukabidhiwa kwa walimu pamoja na baba na mama lishe wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ambapo ametumia nafasi hiyo kusisitiza matumizi sahihi ya gesi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa mtumiaji

Na; Mwandishi Wetu, Kisarawe

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo wamekabidhi mitungi 700 ya gesi pamoja na majiko yake kwa walimu 500 pamoja na Baba na Mama Lishe 200 yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 50 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani huku kampuni hiyo ikiahidi kufunga mfumo wa gesi katika Shule ya Sekondari Minaki ili waanze kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kutumia kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi hiyo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari Wilaya ya Kisarawe Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema anamshukuru Waziri Jafo, kwa kumpatia nafasi ya kupeleka nishati safi ya kupikia kwa walimu pamoja na Baba na Mama lishe wilayani Kisarawe.

“Oryx Gas tunaamini kwamba ukipika kwa kutumia gesi, inaleta maendeleo mengi kwa jamii yetu. Kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti. Zaidi ya yote ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa.

“Wanawake wanatumia muda mchache kupika hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula, na wanaume pia watajiongezea marks ukiwazadia wamama mitungi ya gesi.Kwa kutumia gesi ya Oryx, Watoto wanakua na muda mwingi zaidi kusoma na sio kwenda kutafuta kuni.”

Amesisitiza kuwa kuanzia Julai mwaka 2021 wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali waliyopokea kutoka kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuwa ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Araman amesema kupitia mipango hiyo Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo si tu mbaya kwa afya bali pia ni hatari kwa mazingira yetu huku akitumia nafasi hiyo kueleza pia Oryx Gas inatekeleza juhudi za kueneza matumizi ya nishati safi kwa Watanzania wengi ipasavyo ambayo ni ndoto kubwa ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema Oryx Gas inatekeleza agizo la Serikali kwa kuhakikisha taasisi zenye watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi kwa kutengeza mifumo salama ya gesi kwa kutumia tenki kubwa ambapo mifumo hiyo inaweza tumika shuleni, kambi za jeshi, vyuo vya polisi, magereza na katika kampuni za uzalishaji.

“ Hii inasaidia kupunguza matumizi ya mafuta machafu kwenye mifumo ya uzalishaji. Oryx Gas Tanzania inajipongeza kwa kujulikana kua kampuni kinara katika usambazaji wa gesi ya kupikia majumbani kwa Watanzania kwa sasa. Sisi Oryx Gas Tanzania tutaendelea kuwekeza zaidi katika kuratibu kubadilisha na kueneza nishati safi kutumika na Watanzania kwa kutumia gesi ya Oryx kwa manufaa yetu wote.”

Pia amehimiza wananchi kutumia gesi ya LPG katika shughuli zao mbalimbali ili kuleta maendeleo katika nchi ya Tanzania na kwa ajili ya kuboresha Maisha yetu kiujumla huku akitumia nafasi hiyo kueleza Waziri Jafo amekuwa balozi mzuri wa kuleta maendeleo kwa waalimu na jamii kiujumla kwa kuunga mkono katika mpango huo wa matumizi ya nishati safi wilayani Kisarawe.

Akizungumzia kuhusu kufunga mfumo wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya sekondari ya Minaki , Aramn amesema watafunga mfumo huo ili shule hiyo kuondokana na kutumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na kwamba Orxy itafunga mfumo wenye uwezo wa kubeba ujazo wa tani moja ya gesi na ametoa ahadi hiyo baada ya Waziri Jafo kutoa ombi kwa kampuni hiyo kufunga mfumo huo katika shule hiyo ambayo yeye amesoma kidato cha tano na sita.

Kwa upande wake Waziri Jafo ametumia nafasi hiyo kuishukuru Oryx kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa vitendo huku akieleza kuwa tayari Serikali imeshatoa maelekezo kuanzia mwaka huu wa 2023 taasisi , mashirka na maeneo ambayo yana watu kuanzia 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo nishati ya gesi.

Akizungumzia zaidi Waziri Jafo amesema mbali ya kugawa mitungi ya gesi kwa walimu 500 bado ataendelea kuzungumza na wadau ili apate mitungi mingine kwani lengo lake ni kuhakikisha walimu wote 1300 walioko katika wilaya hiyo wawe wamepata mitungi ya gesi.

“Idadi ya walimu waliko Kisarawe ni 1300 hivyo baada ya kugawa majiko 500 yatahitajika tena majiko 800 ya gesi lakini hili suala tutaendelea kuwafikia wadau .lengo langu kila mwalimu wa Kisarawe awe na gesi. Pia nimemuomba Mkurugenzi wa Oryx atufungie mfumo wa gesi katika sekondari yetu ya Minaki na amekubali na huu ni mwanzo tu kwani nataka kuona shule zote za Kisarawe tunafunga mfumo huo ili kuondakana na matumizi ya kuni na mkaa,”amesema Waziri Jafo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea ORYX YAKABIDHI MITUNGI YA GESI NA MAJIKO YAKE 700 KISARAWE,KUFUNGA MFUMO WA GESI MINAKI SEKONDARI