Timu ya Taifa ya Cape Verde imeiduwaza Timu ya Taifa ya Ghana kwa kuichapa mabao 2-1 katika mchezo wa michuano ya AFCON yanayofanyika nchini Ivory Coast.
Cape Verde ndio walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za mpinzani wake na kupata goli la kuongeza kupitia kwa mchezaji wake Jamiro Montero katika dakika ya 17 ya kipindi cha kwanza cha mtanange huo.
Iliwalazimu Ghana kuaubiri hadi kipindi cha pili kujiuliza na kujipanga, ambapo mlinzi wa Kati wa timu hiyo anayekipiga kwenye Klabu ya Fenabache ya Uturuki Alexander Djiku alipachika bao la kusawazisha kwa kuunganisha mpira wa adhabu akipiga kichwa katika dakika ya 57 ya kipindi cha pili cha mchezo huo.
Cape Verde walifanya mabadiliko katika eneo la kiungo mshambuliaji, ambapo Rarry Rodrigues aliingia na kuongeza kasi ya mchezo na kufanikiwa kushindilia msumari wa pili dakika ya 90 baada ya kupangua safu ya ulinzi ya Ghana na kumfanya mlinda mlango Richard Afori kukosa cha kufanya.
Mchezo huo wa kundi B, umepigwa katika Dimba la Felii Ufubwanyi na kuifanya Cape Verde kushika nafasi ya kwanza kwa kuongoza kundi hilo akiwa na alama 3, ikifuatiwa na Msumbiji na Egypt wote wakiwa na alama 1, huku Ghana akishika nafasi ya 4 katka kundi hilo.