Home LOCAL WAHITIMU CHUO KIKUU MZUMBE WATAKIWA KUWA WAZALENDO

WAHITIMU CHUO KIKUU MZUMBE WATAKIWA KUWA WAZALENDO

Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wametakiwa kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa pamoja na kutumia maarifa na ujuzi waliopata kwa kuleta maendeleo katika jamii.

Wito huo umetolewa leo Desemba 14, 2023 na Rais wa Zanzibar Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Ali Mohamed Shein wakati wa Mahafali ya 22 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mohamed Shein amesema kuwa kujiamini, kufanya kazi kwa bidii ni njia pekee itakayowafanya wahitimu kuaminiwa katika maeneo mbalimbali katika utekelezaji wa mujukumu.

“Wahitimu tunapaswa kujikita katika kufanya tafiti ili kusaidia jamii pamoja na kuangalia mslahi ya jamii pamoja na chuo katika utekelezaji wa majukumu yenu, pia tujiunge mtaandao wa Chuo ili tuweze kukisaidia chuo chetu.” amesema Dkt. Mohamed Shein.

Aidha Dkt. Mohamed Shein amewapongeza watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utendaji.

Amesema kuwa wakati umefika wa kuongeza kasi katika utendaji wa majukumu ili vijana waweze kupata maarifa ambayo yatawasaidia katika kufikia ndoto zao pamoja na kutatua matatizo katika jamii.

Dkt. Mohamed Shein amewakumbusha menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kutumia fursa katika Mkoa huo ikiwemo kuendeleza ya ardhi ya Chuo ili kuongeza mapato.

“Tujenge ukumbi ambao unaweza kukidhi mahitaji chuo jambo ambalo lisaidia kuongeza mapato ya serikali” amesema Dkt. Mohamed Shein.

Kaimu Makamu Mkuu Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha, amesema kuwa wanaendelea kufanya kazi kwa uweledi mkubwa ili kufikia malengo ya chuo.

Amesema kuwa chuo kinatekeleza miradi 17 ya utafiti katika nyanja mbalimbali pamoja na kuchapisha majalada ndani na nje ya nchini.

“Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kimekuwa na utamaduni kutoa huduma za kijamii bure ikiwemo kununua kadi 35 za bima ya afya kwa watoto katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili”amesema Profesa Mwegoha.

Amesema kuwa ili kuongeza ufanisi wamekuwa na programu ya kuwajengea uwezo wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini.

Profesa Mwegoha amewataka wahitimu
554 wa ngazi mbalimbali Ndaki ya Dar es Salaam kuwa wabunifu pamoja na kujiendeleza kitaaluma.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Profesa Saida Yahya-Othman amesema kuwa amewakumbusha wahitimu umuhimu kuongeza maarifa utafiti, uchambuzi wa mambo mbalimbali bila kuumbishwa na mtu yoyote.

Profesa Othman amewataka kwenda kuishi kwa kuzingatia hali ya kipato halisi katika maisha pamoja na kutetea na kukosea inapobidi katika jamii.

“Tukaishi kwa kipato halali bila kufanya uharibifu wowote katika maisha na utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku kazi” amesema Profesa Othman.

Amesema kuwa ukuaji wa teknolojia ya akili bandia umeleta changamoto katika soko la ajira, hivyo nendeni katika jamii kwani tumejifunza kwa maendeleo ya watu.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Bw. Jonas Baraka ametoa shukrani kwa menejimenti na wote walichangia katika safari ya kufanikisha ndoto ya kuongeza elimu katika Chuo Kikuu Mzumbe.

“Wahitimu wa shahada ya awali Ndaki ya Dar es Salaam, Tegeta tunatoa shukrani kwa msaada wenu ambao umeleta ufanisi na tija katika kipindi chote, haikuwa kazi raisi, hivyo tunawapongeza” amesema Bw. Baraka.

Bw. Baraka ametoa wito kwa wanafunzi wanaendelea na masomo kuwa na ushirikiano wa kutafuta ushauri wa wataalamu katika fani wanazosoma.

Chuo Kikuu Mzumbe : Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.

Previous articleWAZIRI MKUU AZINDUA KANZIDATA YA MADEREVA WA CHAMA CHA WAMILIKI WA MALORI
Next articleARDHI SACCOS YATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU KULETA MAENDELEO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here