Dar es Salaam, Tarehe 1 Desemba 2023
Mhe. Mary Chatanda, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ametoa pongezi kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke (TRRH) kwa juhudi zao za kusimamia na kuboresha huduma za afya. Katika ziara yake ya leo katika hospitali hiyo, Mhe. Chatanda ameelezea kufurahishwa kwake na maendeleo na ubora wa kazi inayofanywa na wataalamu na uongozi wa hospitali.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Mhe. Chatanda alisisitiza umuhimu wa kazi inayofanywa na wataalamu na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, akielezea jinsi wanavyoshirikiana kwa uaminifu na kwa uangalifu mkubwa katika kusimamia na kuboresha majengo ya hospitali. Aliongeza kuwa ubora wa huduma unatokana na juhudi zinazofanywa na wafanyakazi wote kwa pamoja.
Ziara hiyo ilihusisha pia Naibu Mwenyekiti wa UWT, Mhe. Zainab Shomari, pamoja na Katibu Mkuu wa UWT, Mhe. Jokate Mwegelo, na viongozi wengine wa UWT. Walipata fursa ya kutembelea Wodi za kina mama waliojifungua na wale wanaosubiri kujifungua, ambapo walishuhudia juhudi za hospitali katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.