Home LOCAL SHILINGI BILIONI 1.4 ZITATUMIKA KUMALIZA KERO YA MAJI KATA YA LIKOKONA NA...

SHILINGI BILIONI 1.4 ZITATUMIKA KUMALIZA KERO YA MAJI KATA YA LIKOKONA NA KAMUNDI WILAYANI NANYUMBU MKOANI MTWARA

CHANGAMOTO ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji vya Kamundi na Likokona wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara, inakwenda kuwa historia kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira kuanza ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji hivyo.

Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Rogers Lyatuu alisema,serikali imetoa kiasi cha Sh. bilioni 1.4 ambapo Sh.milioni 800 zitatumika kutekeleza mradi wa  maji Kamundi na Sh.milioni 600 kwa mradi wa Likokona.

Lyatuu alieleza kuwa,ujenzi wa mradi wa  Kamundi unahusisha ujenzi wa vituo 13 vya kuchotea maji,ujenzi wa tenki moja lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 na ujenzi wa miundombinu mingine na utakamilika mwishoni mwa mwezi huu  na utanufaisha zaidi ya wananchi  3,500 vijiji viwili vya Kamundi na Mkambata.

Kwa upande wa mradi wa Likokona alisema,kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa vituo saba vya kuchotea maji,tenki la ujazo wa lita 100,000 ujenzi wa chanzo (Intake)miundombinu ya maji na utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 3,500.

Kwa mujibu wa Lyatuu,miradi hiyo itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 47  ya sasa hadi kufikia asilimia 65 katika wilaya nzima ya Nanyumbu.

Baadhi wa wananchi wa kijiji cha Kamundi kata ya Kamundi wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,wakimsikiliza kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Nanyumbu Mhandisi Rogers Lyatuu kuhusiana na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji ya bomba unaotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 800
Aidha alisema,kabla ya Ruwasa haijaanza majukumu yake mwaka 2019,upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya ya Nanyumbu ulikuwa asilimia 39,lakini kwa muda wa miaka minne huduma  ya maji imeongezeka na kufikia asilimi 47.

Katika hatua nyingine Lyatuu alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ruwasa wilaya ya Nanyumbu imetengewa Sh.bilioni 2.08 ambazo zitatumika kutekeleza miradi  8 itakayowanufaisha zaidi ya wananchi 23,000.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kutoa fedha hizo ambazo zimewezesha Ruwasa kutekeleza miradi hiyo itakayo maliza kabisa adha ya maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji hivyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kamundi Said Mlaponi,ameishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya bomba ambao unakwenda kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho.

Diwani kata ya Kamundi Elvani Mussa,ameitaka serikali kupitia Ruwasa kumsimamia kwa karibu mkandarasi anayejenga mradi huo ili akamilishe kazi kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.

Ameiomba serikali kupeleka huduma ya maji katika vijiji vinne kati ya vitano vya kata hiyo ambavyo hadi sasa havijapata mtandao wa maji ya bomba ili kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo waweze kuondokana na adha kubwa ya maji safi na salama.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Likokona Ismail Sikumoja amesema,kutokana na ukosefu wa maji safi na salama wananchi wa kijiji hicho wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili yanayopatikana umbali wa kilomita 1 hivyo kuathiri ushiriki wao kwenye kazi za maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here