Home LOCAL SERIKALI YAKABIDHI DAWA NA VIFAA TIBA VYA ZAIDI YA BILIONI 1.61 MVOMERO

SERIKALI YAKABIDHI DAWA NA VIFAA TIBA VYA ZAIDI YA BILIONI 1.61 MVOMERO

Na:  MWANDISHI WETU

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amefunga kazi Mvomero kwa serikali kukabidhi dawa na vifaa tiba vya zaidi ya sh. bilioni 1.61.

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judithi Nguli wakati Bohari ya Dawa (MSD), ilipokabidhi dawa na vifaa tiba vya zaidi ya sh. bilioni 1.61 kwa vituo vya afya na hospitali za wilaya hiyo.

Alisema, hatua hiyo ya Rais Dk.Samia kwa Mvomero ni funga kazi kwani haijawahi kutokea na ameonyesha uzalendo na utendaji wa vitendo katika kumaliza kero ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma na binafsi.

“Tunaomba tumshukuru mheshimiwa Rais ametushusha mzigo wa maswali wasaidizi wake, tunatamani Watanzania wajue kuwa wana Mvomero tuna furaha sana jambo hili ni kubwa pia ameturahisishia utendaji kazi na kutujengea heshima kwa wananchi,” alisema.

Judithi alisema, wilaya hiyo Jiografia yake kila mmoja anaitambua kwanza ni ya kimkakati na pia ni wilaya inayozungukwa na maeneo mengi muhimu ya kiuchumi.

“Wingi wa wananchi wanaohitaji huduma na mahitaji ni makubwa sana tulikuwa tunasubiri kwa hamu vifaa hivi aliwahi kusema kuwa vilio vya dawa sasa basi ametimiza ahadi kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kutenda kupitia MSD,” alisema.

Aliwataka watendaji wa halmashari na hospitali kwa ujumla kuzingatia maadili ya utendaji kazi na kutomuangusha Rais kwa kuhudumia wananchi ipasavyo.

Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kuhimiza utunzaji wa vifaa tiba vilivyotolewa kwani maboresho ya afya yanayofanyika ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.

Alisema hatua ya MSD kutoa dawa na vifaa tiba hivyo kwa mkopo imeacha alama kwa wilaya hiyo, kwani maeneo ya Mvomero ukitoka Gairo hakuna hospitali nyingine ya wilaya.

Alieleza kuwa maeneo ya karibu ikiwemo Dumila na Tuliani yanategemea huduma hizo Mvomero na vipo viwanda kikiwemo cha Mkulazi kilichopo Kilosa, Nguruira na Mtibwa ambapo watumishi wake inapotokea changamoto wanatibiwa katika hospitali hiyo.

“Mbali na viwanda kuna magereza matatu na wananchi wengi wanaokuja kwa ajili ya kilimo ambapo kuna mashamba makubwa ya umwagiliaji huku pia inapotokea ajali katika barabara kubwa inayounganisha Mvomero na mikoa mingine hakuna huduma katika chumba cha kuhifadhia maiti hivyo ujio wa majokofu ya kuhifadhi maiti ya kisasa katika hospitali tatu za Mvomero ikiwemo ya wilaya ni muhimu sana sana,”alisema.

Naye Mbunge wa Mvomero Jonas Zeeland alisema, wananchi wa Mvomero wana deni kubwa kwa Rais Dk.Samia mwaka kwani ujio wa dawa na vifaa tiba hivyo vya zaidi ya sh. bilioni 1 utasaidia kutatua changamoto za wilaya hiyo.

Alisema kwa muda mrefu kulikuwa na majengo ya vituo vya afya vilivyojengwa na wananchi na vile vilivyojengwa na serikali lakini hakukuwa na huduma kutokana na kukosa vifaa tiba.

“Ujio wa vifaa hivi vitasambazwa maeneo yote hususani ya vijijini na baada ya muda mfupi vitaanza kufanya kazi na wananchi kupata huduma huku pia majokofu yaliyoletwa kwa ajili ya kuhifadhia maiti ni muhimu kutokana na jiografia yetu ambapo tumekuwa tukipokea majeruhi na vifo vingi vya ajali ambapo maiti zilikuwa zikipelekwa mkoani,” alisema.

Zeeland alisisitiza kuwa, majokofu hayo yatatolewa katika maeneo mbalimbali na vifaa tiba vingine na dawa zitasambazwa hadi katika vituo vya afya vipya ambavyo ujenzi wake unaendelea kukamilika kikiwemo kituo cha Mlali, Dakawa na Mziha.

Alisema, mabadiliko makubwa yanayofanywa na serikali ya Rais Dk.Samia katika bohari ya dawa matunda yake yameanza kuonekana hivyo wanampongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai kwa kukubali mabadiliko na kuyafanyia kazi kwa maslahi ya wananchi

Kwa upande wake Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Betie Kaema, alisema mbali na dawa na vifaa tiba hivyo Mvomero na maeneo mengine watarajie mambo makubwa zaidi kutokana na maboresho sekta ya afya yanayoendelea kufanywa na Wizara.

“Chini ya Rais Dk.Samia tutarajie makubwa zaidi mpango mkakati uliopo ni kuona dawa na vifaa tiba vinakuwa vya kutosha na kuwapo na akiba katika hospitali na vituo vyetu vya kutolea huduma, kwa sasa tumeanza kuleta vifaa vya afya mara sita kwa mwaka huku maboresho mengine yakiendelea,” alisema.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk.Philipina Philipo aliahidi kwenda kusimamia watoa huduma ipasavyo hususani kwa huduma ambazo zilikuwa hazijawahi kutolewa tangu Uhuru ikiwemo za chumba cha kuhifadhia maiti, oparesheni kwa baadhi ya maeneo na huduma za kibingwa katika afya ya uzazi kwa mama na mtoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here