Issa Sabuni na Zuena Msuya, Morogoro
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya umeme nchini ili itumike kwa muda mrefu.
Amesema hayo tarehe 29 Novemba, 2023 mkoani Morogoro wakati akiwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Vijiji vya Maseyu na Newland vilivyopo katika Kata ya Gwata na alipofanya ziara ya kukagua utejekezaji wa Miradi ya kusambaza Umeme Vijijini inayoratibiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani humo.
Amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika Utekelezaji wa Miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini kwa lengo la kuharakisha maendeleo kwa Wananchi, hivyo wanapaswa kusaidia kulinda miundimbinu hiyo ili iwanufaishe wananchi wengi na kwa muda mrefu.
“Msiruhusu upenyo wa mtu yeyote kuhujumu miundombinu, tuhakikishe tunailinda kwani serikali imewekeza fedha nyingi na tuipe thamani inayostahili”, amesema Naibu Waziri Kapinga.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. SamiaSuluhu Hassan imejipambanua kwa kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuweka miundombinu wezweshi ili waweze kushiriki shughuli mbali mbali za uchumi.
Serikali ya Awamu wa Sita ni ya maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kutumia huduma ya upatikanaji wa umeme vijijini kujiinua kiuchumi kwa kuutimia katika shughulli za biashara.
Naibu Waziri Kapinga amewataka wakandarasi wanaojenga miradi ya REA kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati ili ifikapo Juni 2024 miradiyote iwe imekamilika.
Akielezea utekelezaji wa miradi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema Serikali imewekeza jumla ya shilling 114.6 Billioni kwa miradi mitano inayotekelezwa kwa Mkoa wa Morogoro
Amesema Serikali kupitia REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni yakutekeleza miradi mbalimbali ya umeme ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Mhandisi Olotu amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya vijiji 669 ambapo hadi kufikia sasa vijiji 583 sawa na asilimia 87.1% vimepata huduma ya umeme kupitia mitano.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II), Mradi wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Ifakara, Mradi wa ujazilizi (Densification IIB), Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodimidogo na maeneo ya kilimo na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mhe. KhamisTaletale aliishukuru Serikali kwa utekelezaji wa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Nishati Vijijini Jimboni Kwake.